Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imepata uongozi mpya.
Hii hapa taarifa kama inavyoripotiwa na mwandishi wa TriGen Media, Zulfa Mfinanga, kutoka Arusha…
Taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo mapema wiki hii inamtaja Jaji Blaise Tchikaya kama Rais atakayehudumu kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Rais anayeondoka, Jaji Modibo Sacko, aliyechaguliwa Juni 2, 2025 kwa kipindi cha miaka miwili.
Hata hivyo, Jaji Sacko ataendelea kubaki katika benchi la Mahakama kama Jaji, akiendelea kuchangia utoaji wa haki ndani ya chombo hicho cha Umoja wa Afrika (AU).
Katika hotuba ya kuaga, Jaji Sacko amewashukuru majaji wenzake, Msajili, wafanyakazi na wadau wote wa Mahakama kwa ushirikiano wakati wa uongozi wake.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Rais mpya, Jaji Tchikaya, raia wa Congo Brazzaville, amesema amelipokea jukumu hilo kwa heshima kubwa akiwa na dhamira ya kuendeleza misingi ya Mahakama.
Amesema wakati Mahakama ikijiandaa kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, kuna umuhimu wa kutafakari mafanikio yaliyopatikana na kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuimarisha zaidi ulinzi wa haki za binadamu barani Afrika.
Kwa niaba ya Mahakama, Jaji Tchikaya amempongeza na kumshukuru Jaji Sacko kwa uongozi thabiti na mchango wake katika kuimarisha taasisi hiyo.

Ofisi mpya ya uongozi sasa inaundwa na Jaji Tchikaya (Rais) na Jaji Bensaoula Chafika wa Algeria (Makamu wa Rais).
Jaji Tchikaya ni Profesa wa sheria za umma za kimataifa na haki za binadamu mwenye uzoefu mpana wa kitaaluma.
Alichaguliwa kuwa Jaji wa AfCHPR Julai 2018 kwa muhula wa miaka sita. Amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo kuanzia Juni 2021 hadi Julai 2023.

Kwa upande wa Jaji Chafika, ana Shahada ya Uzamivu katika Sheria ya Umma na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu katika mahakama na utawala nchini Algeria pamoja na kuwa mhadhiri na mshauri wa masuala ya sheria.
AfCHPR ni chombo cha AU kilichoanzishwa kulinda na kuimarisha haki za binadamu na watu barani Afrika, ikiundwa na majaji 11 ambao hukutana mara nne kwa mwaka katika vikao vya kawaida na inapobidi, vya dharura.



