Friday, May 29, 2026
spot_img

REA yaandika historia Tanzania

Usiku unapoingia Namtumbo, mwanga wa umeme unakata giza lililozoeleka. Tabora, majiko mapya yanazima moshi uliokuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Katika maeneo haya mawili tofauti, Tanzania inaandika sura mpya—ambapo nishati si ufahari tena, bali chombo cha maendeleo.

Fuatana na Mwandishi wa masuala ya nishati wa TriGen Media kwa undani wa taarifa hii…

Ni pande mbili tofauti za Tanzania; upande wa magharibi na upande wa kusini, zinazotengenishwa na maelfu ya kilomita, lakini kazi moja tu inafanywa; mapinduzi ya uchumi wa Watanzania kupitia nishati safi.

Wananchi wa Namtumbo mkoani Ruvuma wakifuatilia mkutano wa maofisa wa REA na Mbunge wao

Serikali imelikasimisha jukumu lake hili kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), nao REA hawajaiangusha hata kidogo kwani wanaendesha mkakati kabambe wa kupanua upatikanaji wa nishati maeneo ya vijijini—kuanzia umeme hadi nishati safi ya kupikia.

Ndani ya mkakati huo, Wilaya ya Namtumbo iliyoko Ruvuma kusini mwa Tanzania na maeneo kadhaa ya Mkoa wa Tabora uliopo magharibi mwa nchi zinajitokeza kama vielelezo hai vya mabadiliko yanayoonekana kwa vitendo.

Wilayani Namtumbo, Serikali imewekeza Sh bilioni 12.1 katika miradi ya kusambaza umeme, hatua iliyowezesha vitongoji 307 kati ya 424 kuwashwa umeme, huku vitongoji 79 vikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mbunge wa Namtumbo na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Juma Homera, anasema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wananchi wote wanapata umeme ifikapo mwaka 2030.

“Nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu wa REA (Mhandisi Hassan Saidy) na timu yake kwa kuwezesha vijiji vyote 66 vya jimbo langu kupata huduma ya umeme, na kasi bado inaendelea ya kupeleka umeme katika vitongoji vilivyosalia,” anasema Dk. Homera.

Anasema wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kwa kufanya ‘wiring’ ili kunufaika na umeme unaotolewa kwa gharama ya ruzuku ya Sh 27,000 tu.

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maofisa wa REA

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu, anasema mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa miradi ya ujazilizi na upanuzi wa miundombinu ya umeme.

“Kati ya vitongoji 424 vilivyopo, vitongoji 307 tayari vina umeme, na vitongoji 79 vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Hali hii itafikisha upatikanaji wa umeme hadi takribani asilimia 91,” anasema Mhandisi Nagu.

Mkazi wa Namtumbo, Hamis Mrope, anasema upatikanaji wa umeme unachochea mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa kuongeza fursa za biashara, kuimarisha huduma za afya na elimu, pamoja na kuboresha maisha ya wananchi.

Simulizi ya Namtumbo inaunganishwa na hatua zinazochukuliwa Tabora, ambako Serikali kupitia REA inasambaza majiko banifu zaidi ya 10,300 kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa nishati safi ya kupikia.

Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu

Ramadhan Mganga, ambaye ni Mhandisi Miradi wa REA, amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh milioni 641 kama ruzuku ya majiko hayo.

“Majiko haya kwa bei ya kawaida ni kati ya Sh 62,000 hadi Sh 70,000, lakini baada ya ruzuku ya asilimia 80, mwananchi atanunua kwa Sh 12,500 tu,” anasema Mhandisi Mganga.

Anasema hatua hiyo inalenga kuboresha maisha ya wananchi huku ikilinda afya na mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Tabora, Amos Ackim, anasema maandalizi yamekamilika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na mradi huo.

Katika taswira pana, Tanzania ina zaidi ya vitongoji 64,000, na katika miaka ya hivi karibuni, maelfu ya vitongoji hivyo tayari vimefikiwa na huduma ya umeme, huku vingine vikiwa katika hatua za mwisho za kuunganishwa kupitia miradi ya REA inayotekelezwa kwa awamu.

Mbunge wa Namtumbo, Dk. Juma Homera akiwa na wananchi na maofisa wa REA wilayni Namtumbo

Hii inaonyesha mabadiliko ya msingi katika namna nishati inavyotazamwa nchini—kutoka kuwa huduma ya mijini pekee hadi kuwa haki ya wananchi wote, bila kujali wanapoishi.

Kadri mwanga unavyozidi kuwaka Namtumbo na moshi kupungua Tabora, ndivyo simulizi ya Tanzania mpya inavyojengwa—ambapo nishati si tena kikwazo cha maendeleo, bali injini ya mabadiliko ya kweli ya kijamii na kiuchumi.

Zinazihusiana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Ungana Nasi Kupitia

0FansLike
0FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Za hivi karibuni