Ni uboreshaji mkubwa wa huduma unaorejesha upya tabasamu la safari salama na uhakika wa kuwahi majukumu kwa wakazi wa Mbezi na Kimara jijini Dar es Salaam.
Fuatana na mwandishi nguli wa masuala ya kijamii wa TriGen Media kwa undani wa habari hii…
Ni Ahadi ya kuanza upya kwa ruti ya kutoka Mbezi Luis – Kimara – Gerezani na Kivukoni mapema mwezi ujao ndiyo inayokoleza matamanio ya maelfu ya wakazi wa magharibi mwa jiji la Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na kampuni maarufu ya usafirishaji abiria jijini Dar es Salaam (UDART) maarufu kama ‘Mwendokasi’ inaonyesha kuwapo kwa mageuzi makubwa ya ndani katika utoaji huduma.
UDART ni miongoni mwa huduma za jamii zilizoathiriwa vibaya na vurugu zilizodumu kwa siku tano zilizoikumba Tanzania kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 2, 2025, kiasi cha kusitisha usafirishaji abiria.
“Kwa sasa tunafanya mageuzi makubwa ya ndani katika mfumo wa utoaji huduma. Tumerejea kwa nguvu kuwahudumia Watanzania.

“SI kwamba tunawapa matumaini hewa, hapana. Tumedhamiria. Na ndani ya siku hizi 100 za Rais Samia (Dk. Samia Suluihu Hassan), UDART mpya imezaliwa ikiwa na huduma bora zaidi,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa UDART, Pius Ng’ingo.
Mapema mwezi huu Rais Samia ametimiza siku 100 akiwa ofisi tangu alipoapishwa kushika kipindi cha pili cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Novemba 2, 2025.
Kauli ya Mkurugenzi Mkuu inaungwa mkono na Ofisa Mkuu wa Fedha (CFO), Emilian Novatus, akisema tayari mabasi 30 yamefungwa injini mpya huku mengine yakiendelea na ukarabati ikiwa ni pamoja na kupakwa rangi.

Mabasi hayo yapo barabarani yakitoa huduma kati ya Mloganzila – Kimara; Kimara – Gerezani na Kimara – Kivukoni.
“Yamerejea kwenye hali nzuri kabisa. Lakini pia yapo mabasi mapya 99 yatakayoanza kutoa huduma muda wowote kuanzia sasa kwa kuwa taratibu za kuyatoa bandarini zimekamilia,” anasema Novatus.
Anasema mabasi hayo mapya na mengine zaidi ya 70 ya zamani yanatarajiwa kuimarisha huduma ya usafirishaji abiria katika korido ya BRT awamu ya kwanza ikiwa ni pamoja na kufungua njia ya Morocco.
“Kurejea kwa kasi ya utoaji huduma kwa njia nzima hakukuja hivi hivi. Ni ‘commitment’ (kujitoa) ya hali ya juu ya Menejimenti na watumishi wote wa UDART.
“Tumejitoa kweli kweli! Tumejibana haswa kuhakikisha maelfu ya Watanzania wanaotumia huduma yetu wanapata kitu kizuri kinachoendana na ukuaji wa teknolojia na kasi ya uchumi ya sasa,” anasema Novatus.
Ofisa Habari wa UDART, Gabriel Katanga, anamuunga mkono Navatus akisema teknolojia iliyoboreshwa inamwondolea usumbufu mteja, kwani si kwamba hahitaji kuwa na tiketi tu, bali hata asipokuwa na kadi atapata usafiri.
“Mteja hana haja ya kupanga foleni kununua tiketi au ‘ku-top up’ (kuongeza salio) kwenye kadi yake. Anachopaswa kufanya ni kuwa na ‘App’ ya ‘Mwendokasi’ kwenye simu janja yake na kupitia humo atafanya malipo kwa urahisi kabisa,” anasema Katanga.

‘App ya Mwendokasi’ inamfanya mteja anunue (alipie usafiri) tiketi akiwa popote na wakati wowote kupitia simu ya mkononi; hivyo kuondoa usumbufu na malalamiko kwa makarani vituo ya kukosekana kwa ‘change’ na mambo mengine, kama ilivyo kwa kadi janja ambazo pia hutoa nafasi kwa mteja kujinunulia huduma bila kuonana na ‘cashier’.
Huduma za usafirishaji abiria kutoka Mbezi na Kimara kuelekea Gerezani, Kivukoni na Morocco zilisimama kuanzia mwishoni mwa Oktoba hadi Desemba 2025, pale Rais Samia alipoelekeza fedha zilizopaswa kutumika katika sherehe za Uhuru zitumiwe kurejesha huduma za jamii na kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa.



