Home Uchumi KAMPUNI KUBWA KUIUZIA BoT DHAHABU

KAMPUNI KUBWA KUIUZIA BoT DHAHABU

0

Miaka michache ijayo Tanzania inatarajiwa kuingia kwenye nafasi 10 bora miongoni mwa mataifa yenye hifadhi kubwa ya dhahabu Benki Kuu baada ya kuanza kwa utekelezaji wa kifungu muhimu cha Sheria ya Madini.

Taarifa ya mwandishi wa TriGen Media wa masuala ya uchumi inaeleza kwa undani.

Ni utekelezaji wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123 ndio utakaoiwezesha Tanzania kufikia ndoto hiyo baada ya Benki Kuu (BoT) kufanikiwa kununua kilo 5.02 kati ya malengo ya kununua kilo sita za dhahabu kwa mwaka wa fedha 2024/25; huku malipo yakikamilika ndani ya saa 24 tu.

Taarifa hiyo imetolewa jijini Dodoma Jumatatu ya Juni 16, 2025 wakati wa hafla ya kusaini mikataba ya BoT kununua dhahabu kutoka katika kampuni tano kubwa za uchimbaji dhahabu nchini.

Mikataba hiyo ilisainiwa mbele ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ikihusiha kampuni za Geita Gold Mine (GGM), Buckreef Gold Ltd na Shanta Ltd.

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (katikati) akiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba (kushoto) na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika picha ya ukumbusho baada ya kushuhudia hafla ya utiaji saini mikataba ya kampuni za uchimbaji madini kuiuzia dhahabu BoT.

“BoT itanunua kiasi kisichopungua asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa,” anasema Mavunde.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwigulu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yanayochochea kukua kwa hifadhi ya dhahabu ya BoT, akisema hali hiyo itasaidia kuimarisha uchumi wa Tanzania.

“Serikali kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kuhakikisha inaiwezesha Benki Kuu katika ununuzi wa dhahabu ili kuongeza akiba ya nchi ya ‘𝙢𝙤𝙣𝙚𝙩𝙖𝙧𝙮 𝙜𝙤𝙡𝙙’.

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (katikati) akizungumza na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kushoto) na Gavana wa Benki, Emmanuel Tutuba

“Ninampongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi mzuri wa sekta ya madini mpaka kufikia hatua hii, ninaamini kwa miaka michache ijayo, nchi yetu itakuwa miongoni mwa zile zenye akiba kubwa ya hifadhi ya dhahabu kupitia Benki Kuu,” anasema Mwigulu.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mavunde, amezipongeza kampuni zote za uchimbaji na usafishaji madini kwa kusaini mikataba hiyo ambayo ina matokeo makubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania na kuchochea uongezaji thamani madini.

Mavunde amesema kwa BoT kununua dhahabu kupitia wachimbaji wadogo na wakubwa kutaiweka Tanzania kwenye ramani ya Afrika kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye hifadhi kubwa ya dhahabu.

Akitoa taarifa ya awali, Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, amesema hatua hii itasaidia kuimarisha uchumi wa nchi na sarafu ya Tanzania.

“BoT imejipanga kukuza hifadhi ya dhahabu kwa kuendelea na ununuzi kila mwaka ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa na hifadhi kubwa itakayoihakikishia Tanzania uchumi imara,” amesema Tutuba.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version