Home Kitaifa ‘HONGERA SERIKALI KUZIOKOA TANAPA, NCAA’

‘HONGERA SERIKALI KUZIOKOA TANAPA, NCAA’

0

Ufinyu wa bajeti uliotokana na ucheleweshwaji wa mafungu ya fedha kutoka Hazina unadaiwa kutumbisha kwa kiasi kikubwa shughuli za uhifadhi na utalii kwa taasisi mbili muhimu katika sekta hiyo; TANAPA na Ngorongoro.

Hii hapa taarifa ya kina kama ilivyoandaliwa na Mwandishi wa TriGen Media wa masuala ya uhifadhi na utalii, Joseph Mwanicheta…

Wadau wa uhifadhi na utalii nchini wameelezea furaha yao baada ya serikali kurejesha uhuru wa kifedha kwa taasisi mbili muhimu za uhifadhi; Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, kupitia Bajeti Kuu ya Serikali aliyoisoma bungeni jijini Dodoma Juni 12, 2025, amependekeza taasisi hizo mbili kukusanya na kutumia sehemu ya makusanyo yao.

Huo unatajwa kuwa uamuzi wenye maslahi mapana kwa taifa kutokana na mateso yaliyopitiwa na wahifadhi kwa karibu miaka 10.

Mwigulu anapendekeza kufanyika kwa marekebisho ya Kifungu cha 9 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura ya 282 pamoja na Sheria ya NCAA.

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

Marekebisho hayo yatawapa uwezo TANAPA) na NCAA kutumia sehemu ya mapato yao moja kwa moja bila kupitia mchakato mrefu wa maombi Hazina.

Kwa miaka kadhaa taasisi hizo kubwa zenye dhamana ya kusimamia uhifadhi na utalii nchini zilikuwa zikilazimika kuwasilisha mapato yao yote kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, kisha kuomba upya; jambo lililosababisha kuzorote kwa shughuli zao muhimu, ikiwemo mapambano dhidi ya ujangili.

TANAPA na NCAA ni taasisi za kimkakati katika sekta ya uhifadhi na utalii, zinazochangia zaidi ya dola bilioni 3.9 kwa mwaka katika uchumi wa taifa.

TANAPA inasimamia hifadhi 21 za taifa zilizotawanyika maeneo mbalimbali nchini, huku NCAA ikisimamia eneo maalumu na la kipekee duniani, Hifadhi ya Ngorongoro na eneo la kimondo lililopo Mbozi mkoani Songwe.

Akiwasilisha hotoba ya bajeti bungeni Juni 12 mwaka huu, Waziri wa Fedha, Mwigulu, amesema marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 yanafuta kifungu kidogo cha 2(b) cha mgao wa asilimia 91 kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali.

Badala yake sasa kinaweka mgao wa asilimia 51 ya mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na TANAPA na NCAA kwenye akaunti ya taasisi hizo zilizopo Benki Kuu ya Tanzania.

Mwiguli ameliambia Bunge kuwa mfumo wa awali wa TANAPA na NCAA kuhifadhi asilimia 51 ya mapato yao utarejeshwa kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Ingawa kiwango kinachoruhusiwa kubaki ni kidogo ikilinganishwa na mfumo wa awali ambapo taasisi hizo zilihifadhi hadi asilimia 91 ya mapato yao, mabadiliko haya yanatarajiwa kuleta manufaa si tu kwa taasisi husika bali pia kwa maslahi mapana ya taifa.

Uhuru wa kifedha katika mfumo wa awali uliwezesha taasisi hizo kuendesha shughuli za uhifadhi na utalii kwa ufanisi mkubwa.

Ngorongoro

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa taasisi hizo, pamoja na furaha yao, wanaamini kuwa ingekuwa vyema iwapo serikali ingeziruhusu NCAA na TANAPA kubaki na asilimia 70 ya mapato yao ili kufanikisha kazi za uhifadhi.

“Elimu ya uhifadhi, magari, watumishi na vifaa vinavyotumika katika ulinzi wa maliasili vinahitaji fedha nyingi,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO), Elirehema Maturo.

Anasema serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa kuhakikisha maeneo hayo yanapata fedha kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na utalii.

“Viongozi wameonesha busara kubwa katika jambo hili, tunawapongeza kwa kulitambua tatizo la mfumo wa sasa wa gharama za uendeshaji na kuahidi kulishughulikia katika mwaka wa fedha 2025/26,” anasema.

Kurejeshwa kwa mfumo huu kunatarajia kusaidia pia kupunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni za utalii, kwani miundombinu mibovu huharibu magari na kuathiri faida za biashara.

Mmoja wa maofisa wa TANAPA aliyezungumza na JAMHURI, amesema mabadiliko hayo yatatoa nafuu katika uendeshaji wa shughuli za taasisi tofauti na ilivyo sasa ambapo shughuli nyingi zinafanyika kwa kusuasua kutokana na kutokuwa na mtiririko mzuri wa fedha.

“Kwa mujibu wa mapendekezo ya marekebisho ya kifungu husika, mgao wa makusanyo ya TANAPA utakuwa hivi; asilimia 51 zitaingia akaunti ya TANAPA, asilimia 40 Mfuko wa Serikali, asilimia tatu itakwenda Mfuko wa Wanyamapori (Wizara) na asilimia sita Mfuko wa Maendeleo ya Utalii ambao pia upo wizarani,” amesema.

Mfuko wa Maendeleo husaidia Wizara na wadau kutangaza fursa za utalii ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza watalii na mapato.

Amesema ilivyo sasa usimamizi wa makusanyo ya maduhuli ulikaimishwa TRA, fedha zote zinapelekwa Benki Kuu na zinafanyiwa mgawanyo kupitia Hazina kama ilivyo makusanyo mengine ya serikali.

Mtendaji wa Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO), Elirehema Maturo

“Marekebisho haya yakiidhinishwa na Bunge yataleta ahueni ukilinganisha na mgao wa ‘OC’ (Other Charges). Ninachokiomba ni serikali iendelee kulipa mishahara,” amesema.

MKURUGENZI wa Taasisi ya Waandishi wa Habari za Jamii za Pembezoni (MAIPAC), Mussa Juma, anasema: “Ninaipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wadau wa uhifadhi na kuja na mapendekezo ya taasisi hizo kuachiwa kiasi cha makusanyo ya fedha.”

Amesema uhifadhi unahitaji fedha kila wakati kwa kuwa huko kuna operesheni nyingi za mara kwa mara ikiwemo masuala ya ujangili ,matengenezo ya magari na mitambo, mafuta na malipo mbalimbali.

Anasema TANAPA na NCAA wanapokuwa na fedha wanakuwa na uwezo wa kutatua na kuendelea kustawisha utalii nchini.

“Mfumo uliokuwapo ulikuwa unachangia kuchelewesha miradi ya maendeleo inayotekelezwa. Ikumbukwe kuwa TANAPA, NCAA, TAWA na taasisi nyingine za uhifadhi kama WMAs ni nguzo muhimu ya ustawi wa utalii nchini zinatakiwa kujengewa mazingira rafiki ili kukuza sekta hiyo,” amesema.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version