Home Uchumi BARRICK-TWIGA KINARA GAWIO SERIKALINI 2025

BARRICK-TWIGA KINARA GAWIO SERIKALINI 2025

0

Kwamba sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika pato la taifa unafahamika, lakini kipya kinachojidhirisha wazi kwa sasa ni kwamba ubia kati ya Kampuni ya Barrick Gold Corporation na Serikali ya Tanzania, unalipa zaidi.

Mwandishi wa TriGen Media wa masuala ya uchumi na uwekezaji, Joseph Mwanicheta, na habari kamili…

Miaka michache iliyopita Serikali ya Tanzania imeingia ubia na kampuni kubwa ya uchimbaji madini duniani, Barrick, kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation.

Ubia huo unaonekana kuendelea kuzinufaisha pande zote mbili na leo, Juni 10, 2025, migodi ya Barrick nchini imetoa gawio la Sh bilioni 93.6 kwa Serikali ya Tanzania, kisha kutunukiwa tuzo ya ushindi wa kwanza, kundi la kampuni ambazo serikali ina hisa chache.

Meneja wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido, ndiye aliyekabidhi mfano wa hundi (dummy cheque) kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa hundi ya gawio kutoka kwa Meneja wa Barrick Tanzania, Dk. Dk. Melkiory Ngido wakati wa hafla ya Siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam

Hii si mara ya kwanza kwa Barrick kushika nafasi hiyo kwani katika mwaka wa fedha 2022/23, ilitoa gawio serikalini la Sh bilioni 84 na kupewa tuzo ya ushindi wa kwanza katika kundi husika.

Mwaka wa fedha 2023/24, Barrick ilishika nafasi ya pili iliotoa gawio la Sh bilioni 53.482.

Barrick na Twiga Minerals inamiliki migodi ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ambao upo katika mchakato wa kufungwa.

Akizungumzia mafanikio haya, Meneja wa Barrick Tanzania, Dk. Ngido, anasema mbali na kutoa gawio nono kwa Serikali, Barrick na Twiga wamekuwa wakichangia kukuza uchumi wa taifa kupitia malipo ya tozo, kodi, ushuru, magawio, mishahara na malipo kwa wazabuni wa ndani katika maeneo ya uchimbaji dhahabu.

“Uwekezaji wa Barrick nchini unaendelea kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yanayozunguka migodi kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR),” anasema, akitoa mfani wa jamii inayoishi jirani na North Mara na Bulyanhulu.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, anasema Kampuni ya Twiga Minerals imekuwa ikifanya vizuri kwenye sekta ya uchimbaji madini nchini kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Mchechu anasema kwa mwaka huu, serikali imepata Sh trilioni 1.28 kama gawio, michango na makusanyo mengineo zitakazoboresha sekta za elimu, afya, miundombinu sekta nyingine mtambuka.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version