Home Makala & Uchambuzi MFAHAMU DENNIS, KIJANA ALIYEPAMBANA BILA WAZAZI HADI UHANDISI

MFAHAMU DENNIS, KIJANA ALIYEPAMBANA BILA WAZAZI HADI UHANDISI

0


“Tangu kuzaliwa kwangu sijawahi kumfahamu baba yangu mzazi. Ninaambiwa kwamba mama aliniacha kwa bibi nikiwa na umri wa mwezi mmoja tu! Nikalelewa na kukulia huku kwa bibi.”

Fuatana na mwandishi wa TriGen Media, Egidia Vedasto kutoka Arusha, kwa undani wa simulizi ya kijana aliyepigania maisha kutoka mtaani hadi kuwa mhandisi…

Ni safari ngumu lakini yenye mafanikio. Haikuwa safari rahisi ila kutokana na tamaa ya kuiona kesho yako ikiwa bora, lazima upambane.

Duniani wapo watu waliotoka katika familia duni na kukulia katika maisha ya dhiki, lakini leo wana mafanikio makubwa na ushawishi kwa wengi.

Miongoni mwao ni Barack Obama, Nelson Mandela, Abraham Lincoln, Jay-Z, Oprah Winfrey, Steve Jobs, Ralph Lauren na Andrew Carnegie.

Oprah alizaliwa katika familia maskini huko Mississippi, Marekani, akalelewa na bibi yake baada ya kutelekezwa na mama yake akiwa mchanga!

Akaishi kwenye mazingira yasiyo na matumaini, mara kwa mara akiishi mitaani baada ya kutoroka nyumbani.

Leo hii Oprah ni mmoja wa wanawake maarufu wenye ushawishi mkubwa duniani.

Sasa hapa tunayatazama maisha ya Msimamizi Mkuu wa Karakana ya Kiwanda cha Sunflag, Dennis Laswai (27) mzaliwa wa Rau, Moshi ambaye kwa sasa ni mkazi wa Themi jijini Arusha.

Dennis Laswai akiwa kazini

Historia ya maisha yake inasisimua na imejaa mafunzo lukuki; inatoa mwanga na chachu ya kusonga hata ukiwa katika nyakati ngumu.

Akizungumza na TriGen Media, Dennis anasema alihamia jijini Arusha akidhani kuwa angekutana na bibi yake mdogo aliyekuwa akiishi Arusha wakati ule.

Kwa nini akimbilie Arusha? Anajibu akisema: “Ugumu wa maisha. Maisha yaliongezeka ugumu baada ya mlezi wangu (bibi yake) kufariki dunia.

“Ninaambiwa mama aliniacha kwa bibi nikiwa na mwezi mmoja tu akaenda kusaka maisha kusikojulikana.”

Safari kutoka Rau ilimfikisha Stendi ya Mabasi Moshi, akaulizia yalipo mabasi ya kwenda Arusha, akaelekezwa, akapanda na kufungua ukurasa mpya wa maisha.

Dennis, mtoto wa pili kati ya wanne katika tumbo la mama yake, anasema yeye na ndugu zake hawakulelewa pamoja; kila mmoja alililewa na ndugu mwingine wa mama.

“Kaka yangu alikuwa akiishi kwa bibi mdogo (mama mdogo wa mama yakae) Arusha. Nikalazimika kutoroka kutafuta unafuu wa maisha.

“Tulipofika stendi ya Arusha, watu wakashuka kwenye gari, na mimi nikashuka. Wala sikuombwa nauli labda ilikuwa kutokana na umbo langu. Wakati huo nilikuwa miaka tisa tu.

“Akili yangu siku zile nilidhani nikifika tu stendi Arusha, nitamwona bibi anipeleke kwake. Badala yake, nikakuta watu wengi ambao siwajui kabisa!

“Nikaanza kutemebeatembea tu mitaani, nikiulizwa nipo na nani, ilibidi nidanganye kuwa nimepotezana na mama yangu baada ya kufika stendi.

“Usiku ulipoingia, nilikutana na watoto wengine wakizunguka mitaani kama mimi, nikajiunga nao. Usiku ulipokolea, tukatafuta maboksi tulale.

“Vyumba vyetu vilikuwa vibaraza vya fremu za maduka. Nilipoamka asubuhi, nikakuta wenzangu wamenivua viatu na kuondoka na mfuko wa nguo zangu,” anasema.

Hata hivyo, anasema kutokana na utoto, Aliona maisha ni mzuri tu tofauti na aliyokuwa nayo baada ya bibi yake kufariki dunia.

Safari hatari ndani ya buti

Anasema amelelewa kwenye vituo kadhaa vya watoto wa mitaani kama Kaloleni CCF, Chiswea, Amani Centre na Dogodogo cha Dar es salaam.

“Mimi na wenzangu tuliwahi kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa kujificha kwenye buti la basi. Hata Dar es Salaam maisha yalikwenda kinyume na matarajio yangu.

“Nikaamua kurudi Arusha, lakini kumbe basi nililopanda sio la Arusha; nikajikuta niko Mbeya!  Nikakutana na Wasamaria wema, nikawaambia nimepoteana na wazazi wangu stendi, wakanisaidia kunipandisha basi la Arusha,” anasema.

Dennis anasema hayo yalimkuta akiwa amekimbia shule ya MEMKWA (elimu maalumu kwa walioikosa) aliyokuwa ameanzishiwa na Kituo cha Amani, Dar es Salaam.

Anusurika kifo mara mbili

Dennis anakumbuka siku yeye na wenzake walipokwenda kulala kwenye korongo, nyuma ya Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, karibu na Kanisa Katoliki.

“Usiku, tukiwa usingizini, maji yakashuka kutoka Meru, yakatusomba! Kwa bahati nzuri tukanusurika kwa kujishika kwenye mizizi ya miti na mawe,” anasema.

Kwa kawaida, kwa mujibu wa Dennis, watoto wa mitaani kila asubuhi husogea stendi na kusimama eneo la ‘pipe’ za kutolea moshi ili kupata joto; au huwasha maboksi na kuota moto.

Anasema siku moja walipowasha moto, mmoja wao, akiwa ameshavuta gundi iliyochanganywa na petroli, akasinzia na kuangukia kwenye moto; akaungua tumboni, kidonda kilichomsababishia kifo.

Watoto wenzake kadhaa wa mitaani ama walikatwa mikono, kufungwa gerezani au kukumbwa na vipigo vikali kutoka kwa wananchi kutokana na uhalifu waliokuwa wakiufanya.

Dennis anakitaja Kituo cha Amani kama ‘mzazi na mlezi’ mwema siyechoka kufuatilia hatua kwa hatua watoto wa mitaani, kuwapa chakula kizuri, nguo na malazi, kikitamani kila mtoto abadilike na kurejea katika familia yake; na kupata elimu.

“Sisi tulikuwa tukiona kama usumbufu tu,” anasema.

Itaendelea Jumatatu ijayo

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version