Home Uncategorized TRA yaja na utaratibu mpya Bandari ya Bagamoyo

TRA yaja na utaratibu mpya Bandari ya Bagamoyo

0

Ni mkakati wa kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji mapato ambapo sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Pwani, imekuja na utaratibu mpya.

Fuatana na mwandishi wa TriGen Media wa masuala ya biashara na fedha kutoka mkoani Pwani

Walengwa ni wafanyabiashara wa mafuta wanaosafirisha bidhaa hiyo kupitia Bandari ya Bagamoyo kutoka Zanzibar ambapo , utekelezwaji w ahatua hiyo unaanza Machi 2026 huu.

Akizungumza na wafanyabiashara wa mafuta, wajasiriamali na wachukuzi mjini Bagamoyo kwa niaba ya Kamishna Mkuu, Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Masawa Masawa, amesema lengo la serikali ni kujenga mfumo rafiki wa ulipaji kodi sambamba na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato.

Mmoja wa wadau wa Bandari ya Bagamoyo akizungumza

“Kwa namna hii tutaboresha mapato ya serikali huku tukiweka mazingira rafiki zaidi kwa wafanyabiashara wanaotumia bandari hii kwa shughuli zao za kiuchumi,” amesema Masawa.

Masawa amekanusha taarifa zinazosambazwa mitandaoni kuhusu kufungwa kwa Bandari ya Bagamoyo akisema inapaswa kupuuzwa.

Amesema serikali inataka kuona wafanyabiashara wanatimiza wajibu wao wa kikodi kwa hiari na uwazi, badala ya kutumia njia zisizo halali kuingiza bidhaa nchini.

Wafanyabiasha wanaotumia Bandari ya Bagamoyo wakifuatilia mkutano wa TRA

“TRA haijafunga bandari. Kulitokea changamoto baada ya wafanyabiashara kuwasilisha malalamiko mbalimbali, Serikali ikaunda timu ya kufuatilia na kupata suluhisho. Kazi hiyo imekamilika,” amesema.

Utaratibu unaotarajiwa kuanza Machi mwaka huu utakuwa nafuu zaidi kwa wafanyabiashara na utaongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato.

Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Masawa Masawa

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema bandari hiyo ni kitovu muhimu cha ajira kwa vijana, ikitegemewa na takribani vijana 400 kiuchumi.

Amesema kusuasua kwa shughuli za bandari katika kipindi cha hivi karibuni kuliathiri mapato ya wananchi na usajili wa wafanyabiashara.

Ndemanga ameipongeza serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto za wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo,  Shaibu Ndemanga 

Meneja Msaidizi wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa mkoani Pwani, Melinda Matinyi, amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuchangia mapato ya serikali, akisema ulipaji sahihi wa kodi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mafuta eneo hilo, Shaban Hamsini, amesema kusuasua kwa shughuli bandarini kuliathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa wafanyabiashara na mapato ya halmashauri.

Naye mchukuzi wa madumu ya mafuta, Wema Abdallah, amesema wamepitia kipindi kigumu cha kukosa kazi kwa zaidi ya miezi miwili, hali iliyosababisha wengi wao kukosa kipato cha kujikimu.

Amesema ni matumaini yao kuwa kuanza kwa utaratibu mpya kutarejesha uhai wa shughuli bandarini na kuwawezesha kurejea kazini.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version