Home Kitaifa HAYA HAPA MAAZIMIO KUBORESHA SEKTA YA KILIMO NCHINI

HAYA HAPA MAAZIMIO KUBORESHA SEKTA YA KILIMO NCHINI

0

Tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru pale kilimo kilipotajwa kuwa ndio uti wa mgongo wa taifa la Tanzania, kwa hakika hali haijabadilika na sasa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) linaazimia kuondoa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo nyeti.

Fuatana na mwandishi wa masuala ya kilimo na mifugo kutoka TriGen Media kwa undani wa habari hii…

Ni katika mkutano wa pili wa Kikundi Kazi cha Kilimo chini ya TNBC ndipo hayo yalipojadiliwa jijini Dar es Salaam; mkutano uliojumuisha viongozi kutoka sekta ya umma na sekta binafsi.

“Kwa kushirikiana na sekta binafsi, tumeona haja ya kushughulikia changamoto zilizopo katika sekta kupitia Baraza hili ambalo Mwenyekiti wake ni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

“Lengo ni kuona changamoto hizi zinaondoka na kukifanya kilimo kuwa na tija zaidi kwa wakulima na kwa taifa zima,” anasema Mwenyekiti wa Kikundi Kazi, Gerald Mweli, ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo.

Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa kutokana na mijadala mbalimbali ni kufanya mapitio ya sera, mikakati, sheria na kanuni za kurahisisha upatikanaji mitaji kwa taasisi za kifedha kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu;

Kuunda kikosi kazi kushughulikia changamoto za aekta ya usafirishaji na usimamizi wa ugavi wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa ajili ya masoko ya nje;

Kuimarisha mfumo wa takwimu za mahitaji na matumizi ya mbegu, Serikali ikiombwa kuendelea kuziwezesha taasisi kama Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kuzalisha mbegu bora zaidi.

Maazimio mengine ni kujenga miundombinu ya umwagiliaji, viwanda na masoko katika maeneo ya kilimo cha mashamba makubwa (block farming) na kuimarisha kitovu cha masoko.

Wajumbe wa mkutano wametoa wito wa kuimarisha na kuboresha mfumo unganishi wa kusimamia sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda vya usindikaji na kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa na mrejesho wa Taasisi ya Afya na Ulinzi wa Mimea (TPHPA) kwa wakulima wa korosho na mazao mengine yanayouzwa katika katika soko la kimataifa.

Mwenyekiti Mwenza wa Kikundi Kazi (sekta binafsi), Mtendaji Mkuu wa TAHA, taasisi inayojihusisha na kuendelea kilimo cha matunda na mboga, Dk. Jacqueline Mkindi, amesema maazimio hayo yatafungua fursa nyingi kwa wakulima na wafanyabiashara wa kilimo nchini.

Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha  Kilimo cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, (katikati) akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa Kikundi Kazi. Kulia ni Katibu Mtendaji wa TNBC, Dk. Godwill Wanga na kushoto ni Mwenyekiti Mwenza (sekta binafsi), Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dk. Jacqueline Mkindi.

“Ninapongeza juhudi za Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kilimo. Miradi kama ya ruzuku ya mbolea, bei nzuri ya mazao na Mpango wa BBT (Jenga Kesho iliyo Bora) ni ya kuungwa mkono,” anasema.

Miongoni mwa maazimio makuu ni kuboresha huduma za ugani, kuhamasisha sekta binafsi kujisimamia yenyewe, kuboresha ulipaji wa ruzuku kwa wakati, kuendeleza sekta ya sukari kwa kukiimarisha Chuo cha Taifa cha Sukari, kuimarisha chuo cha ubunifu na kuweka dirisha na namba moja ya malipo badala ya kila taasisi kudai stahiki yake, ili kuondoa usumbufu.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Dkt. Andrew Komba, amesema taasisi hiyo imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ununuzi wa nafaka kwa bei ya ushindani ili kuwasaidia wakulima.

“Tunawakaribisha wadau wa kilimo kuwekeza kwenye ujenzi wa maghala katika mikoa ya Ruvuma, Songwe na Rukwa, kwani huko tunatarajia kununua tani nyingi za nafaka,” anasema Dk. Komba.

Wakulima wa miwa, pamba, korosho, kahawa na chai walihudhuria na kupata fursa ya kuelezea changamoto wanazokumbana nazo.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version