Padri Felician Venannt Nkwera kuzikwa Jumamosi mei 17 ni huko Ubungo Riverside jijini Dar es Salaam, nyuma ya Kiwanda cha Unga cha Azania, mahala ambapo ndipo kilipo Kituo cha Maombezi cha Mama Bikira Maria (The Marian Faith Healing Centre) kinachoongozwa na Padri Nkwera; ambaye ametangulia mbele za haki.
Fuatana na Mwandishi Maalumu wa TRIGEN MEDIA kwa undani wa habari hii…‘Habemus Papam!’ Jioni ya Mei 8, 2025 itabaki kwenye kumbukumbu ya wengi duniani kwa kuwa ndiyo siku ambayo Kanisa Katoliki lilimpata Papa Leo XIV kufuatia kifo cha Papa Francis kilichotokea Aprili 21, 2025.

Wakati umati wa waumini wa Kanisa Katoliki waliofurika kwenye viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Vatican wakiungana na mamilioni wengine kwingineko duniani kakishangilia habari hiyo njema iliyowekwa hadharani na Kardinali (mwandamizi) Dominique Mamberti; ndani ya chumba kimoja katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam; mmoja wa viongozi wa kiroho mwenye mvuto mkubwa, alikuwa akikata roho.
.“Kwa siku tisa alikuwa amefunga akiomba kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mama Bikira Maria ili Kanisa liweze kumpata Baba Mtakatifu wa mapenzi ya Mungu,” TRIGEN MEDIA imeelezwa.
Kiongozi huyo wa kiroho ni Padri Felician Venant Nkwera, maarufu zaidi kama Fr. Nkwera, aliyekuwa na karama za maombezi na uponyaji.Haijafahamika wazi iwapo Fr. Nkwera alikumbwa na mauti akiwa tayari amelisikia tangazo la ‘Habemus Papam!’ au la; lakini ukweli ni kwamba alikufa wakati enzi mpya za uongozi wa Papa Leo XIV zilipokuwa zikianza rasmi.
Waliokuwa karibu naye katika siku zake za mwisho duniani, wanaamini kwamba Mungu amemchukua akiwa tayari amemaliza moja ya kazi zake kubwa; kuliombea Kanisa kupata Baba Mtakatifu wa mapenzi ya Mungu.“Pamoja na kuzorota kwa afya yake, Mtumishi wa Mungu, Fr. Nkwera, alifunga kwa siku tisa! Kuna wakati wasaidizi wake walimwomba ale (chakula), lakini yeye akasisitiza kuwa lazima aendelee na kufunga,” anasema mmoja wa watu wa karibu.
Kazi nyingine kubwa alizokuwa akizifanya katika siku zake za mwisho ni kuombea Uchaguzi Mkuu 2025 uwe wa amani; ujenzi wa ‘Shrine’ ya Bikira Maria hapa Riverside na Kanisa Kubwa la Mama Maria mjini Tabora.
Hali ilikuwaje kituoni?
Kwa kawaida Riverside huwa hapakauki waumini na Alhamisi ya Mei 8, 2025 watu walikuwapo wakiendelea na ibada, maombi na misa takatifu.
Padre aliyekuwa akitoa huduma za kiriho na kuadhimisha ibada ya misa takatifu asubuhi ya siku hiyo, alimpelekea Fr. Nkwera komunio chumbani kwake.“Baadaye, Baba akatoka, akitembea kwa kutumia fimbo zake mbili na kupanda gari kwenda hospitali akisindikizwa na padri na wasaidizi wengine.“Padri aliyemsindikiza alirudi kituoni na kuadhimisha misa takatifu ya saa 12 jioni.
Tunaomfahamu tulimwona kabisa kuwa hana furaha,” amesema.Saa tatu usiku, padri huyo aliyekuwa akitoa huduma za kiriho kituoni aliondoka ghafla kituoni kwenda TMJ na saa nane usiku wa kuamkia Mei 9, 2025; waumini wakijiandaa kuanza ibada ya Njia ya Msalaba, ndipo ilipotangazwa rasmi kwamba Fr. Nkwera ametwaliwa kwenda kwa Baba!“Kwa sasa tupo kwenye maombolezo na maandalizi. Kama ratiba haitabadilika, basi saa nne ya Ijumaa tutaupokea mwili wa Baba Padri Nkwera kutoka huko uliko.“Tutaupokea pale John Kijazi Interchange (Barabara ya Juu ya John KIjazi), Ubungo na kuuleta hapa kituoni kwa maandamano.

Kutakuwa na Ibada ya Mkesha na Mungu akitujalia, basi tutampumzisha hapa hapa siku ya Jumamosi, Mei 17, 2025,” anasema mjumbe mmoja wa kamati ya maandalizi ya mazishi.Taarifa kutoka TMJ zinasema kwamba jioni ya Mei 8, 2025 kati ya saa mbili na saa tatu usiku, Fr. Nkwera aliwatazama wasaidizi wake, akawaambia: “MSIOGOPE!” Kisha akavuta shuka, akajifunika na akakata roho.
Je, Fr. Nkwera ni nani, ametoka wapi na ameacha nini duniani? Endelea kufuatana na TRIGEN MEDIA hadi Jumamosi baada ya mazishi yake.