Katika kuimarisha uratibu na maendeleo ya sekta ya nishati, Chama cha Wataalamu na Wadau wa Nishati (TEA) kimetakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo, sera na taratibu.
Mwandishi wa TriGen Media katika masuala ya nishatia anaripoti…
Ushauri huo umetolewa na serikali kwa kuzingantia umuhimu wa sekta ya nishati kwa uchumi wa taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, mwakilishi wa Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda, amesema TEA ina mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya nishati kwa kuwaunganisha wadau mbalimbali na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili.
Nyanda amesema wizara inahitaji wadau watakaoshirikiana nayo kwa karibu kusukuma gurudumu la maendeleo ya sekta hii ambayo ni muhimili muhimu wa ustawi wa taifa.

“Sote tunajua umuhimu wa sekta ya nishati. Tunapopata mdau kama chama hiki, ni muhimu kushirikiana na serikali katika kuendeleza ajenda ya upatikanaji wa nishati,” amesema Nyanda.
Nishati inayozungumziwa hapa si umeme pekee, bali pia nishati safi ya kupikia, matumizi bora ya nishati pamoja na sekta ya usafiri.
Wizara inaitazama TEA kama mdau muhimu katika utekelezaji wa ajenda za nishati, hivyo kuongeza wigo wa wadau ili kujenga uelewa mpana kuhusu masuala ya nishati nchini.
Nyanda amesema wanatarajia TEA kusaidia kuwafikia wadau wengi zaidi, kushughulikia masuala ya utafiti na ubunifu, pamoja na kuwa jukwaa la kubadilishana mawazo kati ya serikali na wadau.
“Pia watakuwa jicho pana katika kufuatilia utekelezaji wa mipango ya wizara na kusaidia kurekebisha changamoto zitakazojitokeza,” amesema.

Mwenyekiti wa TEA, George Michael, amesema lengo la kuanzishwa kwa chama hicho ni kuwaunganisha wadau wa nishati wawe na sauti moja katika kuwasilisha hoja, changamoto na mapendekezo kwa ufanisi kabla ya kuwasilishwa katika wizara husika kwa utekelezaji wa sera na sheria.
Michael amewataka wadau wote na vyama vya nishati kujiunga na TEA ili kushirikiana kwa karibu kusukuma maendeleo ya sekta hiyo, hususan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika jamii.
Amesema TEA itakuwa msaada kwa wadau katika masuala ya kisheria, akibainisha kuwa wengi hukumbana na changamoto lakini hukosa mwongozo wa namna ya kupata msaada stahiki.
Kupitia chama hicho, wadau wanaojihusisha na uzalishaji na matumizi ya nishati — ikiwemo gesi ya magari, petroli, oksijeni, biogesi na umeme wa maji (hydro) — pamoja na taasisi kama Tanzania Atomic Energy Commission, watanufaika na mtandao mpana wa ushirikiano na maendeleo.



