Mageuzi ya uchumi wa vijijini nchini yanapaswa kupanuliwa na kuhusisha kikamilifu uchumi wa buluu, ufugaji, misitu na mazao yake ili kuongeza tija na kipato cha wananchi.
Pata taarifa hii kwa undani kutoka kwa mwandishi wa TriGen Media aliyeko Cartagena, Columbia
Akichangia mjadala katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo Vijijini unaoendelea mjini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, amesema mageuzi hayo yatakuwa na maana zaidi yakilenga sekta zenye mguso wa moja kwa moja kwa maisha ya wananchi wa vijijini.

Akiwamkilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo, Profesa Shemdoe amesema mkakati huo unaendana na azma ya serikali kuhakikisha kilimo na ufugaji vinabadilika kutoka shughuli za kujikimu na kuwa vyanzo halisi vya faida kwa wananchi.
“Tanzania inaendelea kukuza uchumi wa buluu kwa kutumia rasilimali za maji kuongeza kipato cha jamii za Pwani, sambamba na kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu ili kuongeza thamani ya mazao yake na kulinda mazingira,” amesema.
Katika kikao cha kujadili maazimio ya mkutano, Profesa Shemdoe amesisitiza umuhimu wa kutambua sekta za ufugaji na uvuvi kama nguzo muhimu za maendeleo vijijini.
Amependekeza kuwepo mkakati mahsusi wa kufuatilia utekelezaji wa maazimio kwa wakati, akionya ucheleweshaji wa tathmini kama ilivyotokea baada ya mkutano wa kwanza mwaka 2006.

Tathmini ya mwaka huo imefanyika katika mkutano wa pili mwaka huu, 2026; miaka 20 baadaye.
Katika hatua nyingine, Profesa Shemdoe ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha pembeni cha uwili kati ya Tanzania na Indonesia, ambapo upande wa Indonesia uliongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Dk. Ir. Sam Herodian.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilijadili kufufua ushirikiano katika kilimo cha mpunga pamoja na kuendeleza ufadhili wa masomo kwa Watanzania nchini Indonesia kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Majadiliano yetu yamepelekea tuanze maandalizi ya rasimu ya hati ya makubaliano kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ubalozi wa Indonesia nchini Tanzania,” amesema Profesa Shemdoe.
Pia amekutana na kufanya mazungumzo na Amy Regas, mwakilishi wa Shirika la Land Facility, ambalo limeonesha nia ya kuifadhili TAMISEMI katika kuandaa mradi mkubwa wa kujengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na biashara ya kaboni.
Mradi huo unatarajiwa kujadiliwa zaidi katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo (Donor Roundtable Meeting) utakaofanyika Mei, 2026.



