Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimewata makada wanaojitikeza kutia nafasi za udiwani na ubunge kuchunga kauli zao na kuzingatia kanuni na sheria za chama katika mchakato wa uchaguzi.

Katika kikao na waandishi wa habari ambapo TRIGEN media ilikuwepo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Salim Abri Asas amebainisha kuwa kutangaza nia ni haki ya wana CCM wote lakini wanatakiwa wafanye kwa staha bila kutoa tuhuma, kejeli, dhihaka au kumtukana mtu mwingine, kwani wote ni wanachama wa CCM.
“Mwanachama anayemtangaza nia anapaswa kufanya hivyo kwa heshima bila kumuumiza mtu mwingine kwa maneno au matendo ya kejeli, dhihaka au unyanyasaji wa aina yoyote,” amesema.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wanachama kuelewa na kuheshimu katiba na kanuni za chama ili kuepuka kuvunja taratibu kwani chama kitahakikisha haki zinafanyika katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yasin, ameonya wanachama wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama kuachana na mienendo na tabia zinazokiuka taratibu za chama.
Amesisitiza kwamba chama kitazingatia haki katika kupitisha majina ya wagombea na kuhakikisha mchakato unafanyika kwa uwazi na uadilifu.
Yasin amesema ni vyema wanachama wasitumie njia zisizofaa au kutekeleza matendo yaliyopigwa marufuku na chama wakati wakitangaza nia zao na CCM itahakikisha kanuni na taratibu zinafuatwa kikamilifu
Kupitia mkutano huo na wanahabari Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa Said Goha amesema kanuni na taratibu za chama hicho ziko wazi ni vema wana CCM wakafahamu na hatua zitachukuliwa kwa wote watakaokwenda kinyume na maelekezo ya chama hicho.