Tuesday, June 17, 2025
spot_img

CHEZA GOFU HUKU UKIFANYA UTALII SERENGETI

Utajisikiaje pale utakapokuwa ukishiriki mchezo wowote iwe wa kimashindano au wa kujifurahisha ilhali ndani ya kilomita moja tu ya mraba, wanyamapori wakiendelea na malisho yao bila hofu yoyote?

Hilo sasa litawezekana nchini baada ya Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kupendekeza kuanzisha bidhaa mpya ya utalii; sports tourism.

Hii hapa makala ya mwandishi wa TriGen Media, JOSEPH MWANICHETA kutoka Fort Ikoma, Serengeti mkoani Mara.

Jeneral(Mstaafu),George Waitara akiwa kwenye Uwanja wa Golf Serengeti

Wakati Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikizinduliwa jijini Dodoma wiki iliyopita na kuelekeza kuwapo kwa mipango ya kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini kutoka milioni tano mwaka huu hadi kufikia milioni nane mwaka 2030, tayari TANAPA inaendelea na ujenzi wa uwanja wa gofu wenye viwango vya kimataifa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).

Viwanja (mashimo) 15 kati ya 18 vya ‘Fort Ikoma Serengeti Golf Course’ vimekamilika na wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi wanaamini utakapofunguliwa na kutangazwa kwa kuingizwa kwenye vifurushi (packages) vya utalii, utakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM iwapo itapata ridhaa ya kuliongoza taifa baadaye mwaka huu; kuongeza idadi ya watalii na mapato kwa taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanapa Investment Company Ltd., Dk. Richard Matolo, ameiambia TriGen Media kwamba gharama za ujenzi wa uwanja pekee ni Sh bilioni 9.5.

“Kwa sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 65 na kazi inaendelea,” anasema Dk. Matolo ambaye ni Mhandisi Mshauri.

Utekelezaji wa mradi wa uwanja ulianza mwaka 2023 na unaweza kukamilika ndani ya miezi sita tu kutokana na upatikanaji wa fedha.

TANAPA Investment Ltd inajenga uwanja huo kwa ushirikiano na washauri kadhaa, wakiwemo wachezaji maarufu wa gofu nchini.

Alama ya Uwanja wa Golf Serengeti uliopo Fort Ikoma,Pembezoni mwa Hifadhi ya Serengeti

Ujenzi wa uwanja wa gofu pembezoni mwa Senapa ni tunda la wazo la Bodi ya Wadhamini ya TANAPA.

“Bodi ilibuni njia mpya ya kuvutia na kuendeleza utalii. Sasa mcheza gofu atalala kwenye nyumba ya kifahari (itakayojengwa eneo hilo), kisha ataelekea Nyatwali (pwani ya Ziwa Victoria). Hapo atapata huduma ya usafiri wa boti ya kasi kwenda Kisiwa cha Saa Nane (Mwanza), Rubondo na Burigi Chato (Geita). Huu ni utalii wa maji.

“Mtalii huyo huyo anaweza kurudi kwa ndege au barabara hadi uwanja wa gofu Serengeti! Hii ni kuongeza thamani ya mnyororo wa fedha za kigeni na mapato zaidi,” anasema.

Kijiografia, Uwanja wa Gofu Serengeti uko nje ya hifadhi na imefanywa hivyo makusudi kuepusha athari zinazoweza kuukumba uhifadhi na mfumo wa ikolojia wa hifadhi hiyo maarufu duniani.

Dk. Matolo anasema uhifadhi ni jambo nyeti na kwamba kutoweka kwa viumbe wakubwa na wadogo kunasababisha madhara duniani.

Uwanja huu umejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na unatarajiwa kuwa wa kipekee duniani – si kwa kuwa uko karibu na hifadhi maarufu duniani, bali pia kwa muundo wake.

“Mradi unatekelezwa katika eneo la ekari 450, utakuwa miongoni mwa viwanja virefu zaidi vya gofu duniani, ukiwa na kilomita 7.065, ambapo mchezaji atatembea kilomita 3.528 kwa mashimo ya ndani na kilomita 3.537 kwa mashimo ya nje,” anasema Dk. Matolo.

Awali, akizungumza eneo la Fort Ikoma wiki iliyopita, mmoja wa wasimamzi wa ujenzi wa uwanja, Zakaria Edward, amesema vikwazo ni miongoni mwa mambo yanayoufanya uwanja wa gofu kuwavutia zaidi wachezaji.

“Nimewahi kucheza gofu katika viwanja vingi, kila kiwanja kina changamoto zake. Uwanja huu una changamoto za ziada; upepo, kwa sababu eneo hili ni la wazi.

“Hapa upepo hubadili mwelekeo mara kwa mara. Mbali na upepo, tutaongeza vikwazo vingine kama mabwawa ya maji na vingine kadhaa,” anasema.

Edward, mchezaji wa gofu wa Klabu ya Lugalo ya Dar es Salaam anasema ili uwanja ubaki katika ubora wake, eneo hilo kumejengwa bwawa la maji na visima viwili vitakavyotumika kusambaza maji.

Anaamini kuwa watalii watavutiwa na uwanja huo kwa kuwa eneo ulipo wanyamapori kama swala na pundamilia hulikaribia na kuonekana kwa urahisi.

Katika kuhakikisha gofu inachezwa majira yote ya mwaka, Edward anasema:

“Mvua huathiri viwanja vya gofu na tumelizingatia hilo. Hapa kutakuwa na mfumo wa mifereji ya maji kuhakikisha mchezo unaendelea hata baada ya mvua kubwa kunyesha.”

Mradi pia unahusisha jengo la kupumzikia wachezaji (club house) ambalo nalo litajengwa.

Pembeni ya Uwanja wa Gofu Serengeti, upo Uwanja wa Ndege wa Fort Ikoma na kwa mujibu wa Dk. Matolo nao ni sehemu ya mradi huo na tayari wageni wanaoshuka na ndege hapo hutembelea eneo la mradi kuona maendeleo ya ujenzi.

Kazi ya utandazaji wa mabomba ya kunyunyizia maji katika kazi ya Ujwanja huo wa Golf ikiendelea.

Wadau wazungumza

Watalii kutoka Boston, Marekani, Paul na Siri Myers ambaoo wapo Serengeti kwenye fungate, wanasema watalii wenye uwezo wa kifedha watafurahia kuwapo kwa uwanja wa gofu.

Kwa upande mwingine, wawili hao walionyesha kufurahia mandhari nzuri ya Serengeti na kuahidi kurudi tena nchini kutalii.

Mwongoza watalii, Peter Lyimo, ambaye yupo katika fani hoyo kwa zaidi ya miaka 30 sasa, anasema:

“Mwanzilishi wa wazo la kujenga uwanja wa gofu Serengeti anastahili pongezi. Hakuna sehemu nyingine duniani ambapo gofu inachezwa huku ukiona wanyamapori. Tutautangaza uwanja huu ili kuvutia watalii zaidi, hasa wawindaji.”

Uwanja wenyewe

Uwanja wa Gofu Serengeti una jumla ya ‘par’ (idadi ya juu ya mipigo inayohitajika katika shimo) 72; mashimo ya ndani yana ‘par’ 36 na ya nje ‘par’ 36.

Uwanja huu una eneo la mazoezi (range) lenye urefu wa mita 430. Kuna maeneo magumu (rough regions) yenye vizingiti kama milima midogo, mabonde, mabwawa ya mchanga (bunkers), na miinuko midogo.

Jeneral (Mstaafu) George Waitara akiwa kwenye Uwanja wa Golf Serengeti

Eneo lenyewe si tambarare. Takriban miti 3,000 ya aina ya ‘acacia tortilis’ itapandwa kuongeza vizingiti (doglegs). Gofu huhitaji umakini mkubwa wa ubongo ili kutumia ‘par’ chache kufikia shimo.

“Kwa sasa, tunaweka mabomba ya daraja la ‘D’ (PVD) kwa ajili ya mfumo wa kumwagilia, ambayo ni sehemu muhimu ya ujenzi. “Mabomba haya yana unene wa sentimita 1, kipenyo kutoka inchi 6 hadi 1.7. Majani ya gofu ya aina ya bamunda na mashine maalumu za kukata yatatumika,” anasema Dk. Matolo.

Anasema mbali na uwanja wa ndege wa Fort Ikoma, jengo la mapumziko, nyumba za kifahari, hoteli na miundombinu mingine vitajengwa kwa kushirikiana na wawekezaji ili kuhudumia wachezaji.

Zinazihusiana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Ungana Nasi Kupitia

0FansLike
0FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Za hivi karibuni