RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Uingereza kuwekeza Zanzibar katika fursa mbalimbali ikiwemo sekta ya uchumi wa buluu, utalii, usafiri wa baharini, uvuvi, nishati na miundombinu ya kidijitali.
Dk Mwinyi amesema hayo alipojumuika kwenye chakula cha jioni na wakurugenzi wa taasisi mbalimbali za biashara na uchumi za Uingereza kilichoandaliwa na Taasisi ya Eastern Africa Association ya Uingereza katika Jiji la London Aprili 7, 2025.
Aidha, Rais Dk Mwinyi amesema katika kipindi cha miaka minne uchumi wa Zanzibar unaendelea kukua zaidi ya asilimia 7 kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta mbalimbali.
Dk Mwinyi ametoa wito kwa wawekezaji hao kuwekeza katika zao la mwani, ameeleza kuwa Zanzibar ndio mzalishaji namba moja wa zao hilo Afrika ambalo soko lake linaendelea kukua zaidi.