Home Kitaifa RITA yagonga hodi kwa viongozi, wazee wa kimila

RITA yagonga hodi kwa viongozi, wazee wa kimila

0

Hakuna atakayeachwa nyuma wakati huu ambapo kasi ya maendeleo ya kiteknolojia ikiendelea ndani na nje ya nchi; awe kiongozi wa kiserikali au wa kimilataasisi za kiserikali pia zikihusika.

Hii hapa taarifa kwa undani kutoka Mpanda mkoani Kativik ama inavyoletwa na Mwandishi wa TriGen Media, Walter Mguluchuma.

Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imetoa mafunzo kwa viongozi wa Serikali na wazee wa kimila kutoka mikoa sita nchini kuwawezesha kusimamia ipasavyo migogoro inayotokana na mirathi, ndoa na talaka katika maeneo yao.

Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Knyasi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina iliyotolewa na mamlaka hiyo kwa  wadau mbalimbali .

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo, Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria katika kushugulikia masuala hayo ili kupunguza migogoro ya kifamilia na kulinda haki za warithi halali.

“Viongozi wa ngazi za msingi wana nafasi ya kipekee katika kutoa elimu kwa jamii na kusimamia utekelezaji wa sheria katika maeneo yao ya kazi na kupunguza migogoro katika jamii,” amesema Kanyusi.

Afisa Msajili Msaidizi Mkuu wa RITA, Victoria Mushi, akitoa elimu ya namna bora ya kuhifadhi wosia, usimamizi sahihi wa mirathi na usimamizi sahihi wa ndoa na talaka.

Amesema kupitia mafunzo hayo ya siku mbili, washiriki watapata fursa ya kujifunza taratibu za uandishi na uhifadhi wa wosia, usajili wa mirathi pamoja na wajibu wa viongozi wa kimila katika kuhakikisha mgawanyo wa mali unafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi.

Wakuu wa Wilaya, maofisa tawala, maafisa tarafa na viongozi wa vitongoji kutoka mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mbeya na Songwe wameshiriki.

Kanyasu amewataka viongozi, pamoja na kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, kutumia busara katika kutatua changamoto zinazoikumba jamii, kwa kuwa wao wako karibu zaidi na wananchi.

Ofisa Msajili Msaidizi Mkuu wa RITA na mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo, Victoria Mushi, ameeleza faida za wananchi kuandika wosia mapema na kuhifadhi nyaraka kwa mujibu wa utaratibu rasmi, akibainisha kuwa hatua hiyo husaidia kuepusha migogoro isiyo ya lazima miongoni mwa warithi pindi mmiliki wa mali anapofariki dunia.

“Tumeshuhudia jamii nyingi zikiingia katika migogoro mikubwa, hususan ya mirathi, na mara nyingi chanzo chake ni ukosefu wa elimu kuhusu uandaaji wa wosia.

“Hivyo, tunaamini kuwa mwendelezo wa mafunzo haya utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro,” amesema Victoria.

Viongozi na wazee wa kimila waliohudhuria mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika Mpanda, mkoani Katavi

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph, amesisitiza umuhimu wa viongozi kutoa mwongozo kwa wananchi kuhusu huduma za RITA zinazopatikana kupitia mfumo wa kidijitali (eRITA), hususan katika usajili wa ndoa, talaka, wosia na udhamini wa mirathi.

“Kupitia mafunzo haya, tutaimarisha uwazi katika utoaji wa huduma sambamba na utoaji wa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi zote za uongozi, ili kulinda haki za wananchi na kupunguza migogoro,” amesema Jamila.

Washiriki wa mafunzo wakifuatilia kwa makini mada zinazotolewa

Miongoni mwa wazee wa kimila walioshiriki, Nelson Majura, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutoa mwongozo sahihi kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kimila katika kusimamia masuala ya mirathi.

Mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa RITA wa kuendelea kutoa elimu kwa umma na viongozi wa ngazi mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha haki, uwazi na utawala bora vinazingatiwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version