Mamia kwa maelfu ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi; wengi wakiongozana na familia zao, wapo nchini kutembelea hifadhi za wanyama za taifa zilizopo kaskazini mwa Tanzania.
Fuatana na mwandishi wa TriGen Media aliyetembelea hifadhi hizo…
Serengeti na Tarangire. Hizi ni miongoni mwa hifadhi maarufu za wanyamapori zilizopo nchini Tanzania zinazosimamiwa na Serikali chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Katika kipindi hiki cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka, mwaka huu hifadhi hizi zinaelekea kuvunja rekodi ya ukusanyaji mapato kutokana na wingi wa wageni wanaozitembelea na kutumia siku nyingi kutalii.
Tayari kumeripotiwa ongezeko la mapato kwa dola za Marekani milioni 20 kati ya Oktoba 1 na Desemba 14, 2025 tofauti na kipindi kama hicho mwaka jana katika Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA) pekee.

TriGen Media imezungumza na Mhifadhi Mwandamizi, Fabian Manyonyi, kwenye lango la kuingia Serengeti la Naabi, akisema katika kipindi hicho, wamekusanya Sh. bilioni 49.2.
“Hili ni ongezeko la asilimia sita kutoka katika makusanyo ya kipindi kama hiki mwaka 2004, ambapo tulikusanya Sh 46.6,” anasema Manyonyi.
Kauli yake inathibitishwa na wingi wa wageni waliokuwapo langoni hapo kukamilisha taratibu za ama kuingia au kutoka hifadhini humo.
Serengeti ni moja ya hifadhi zenye kuvutia barani Afrika ikichagizwa na ukubwa wake, tambarare lakini hasa tukio la uhamaji wa wanyama (great migration) kutoka hapo kwenda Maasai Mara nchini Kenya, na kurudi Tanzania.
Michael Schlittenbaver, mtalii kutoka Ujerumani, anaisifu Serengeti akisema inafikika kwa urahisi; akitaja ukarimu wa Watanzania kama kitu kingine cha kipekee kinachowavutia wageni; na kuahidi:
“Bila shaka nitarudi tena Tanzania na pia nitawashauri ndugu na rafiki zangu waje huku kujionea maajabu ya kuvutia.”
Siri ya mafanikio Serengeti
Mhifadhi Mwandamizi, Manyonyi, hana shaka kwamba Serengeti ipo katika mwelekeo sahihi wa ukuaji, akitaja tuzo za kimataifa inazotunukiwa kama chagizo la kukua kwake.
Serengeti ni mshindi wa Tuzo za ‘World Travel Awards 2025’ ikiwa mbele ya hifadhi maarufu duniani kama Kruger ya Afrika Kusini na Yellowstone ya Marekani.
Pia imetajwa kuwa ‘Hifadhi Bora ya Taifa Barani Afrika’ ikiwashinda washindani wake wakubwa kutoka Botswana, Namibia na Uganda.
Julia Moerer, raia wa Uholanzi, yupo Serengeti akisherehekea miaka 40 ya ndoa ya wakwe zake, anasema Serengeti inavutia kuliko Kruger.
“Nimetembelea Kruger (Afrika Kusini). Huko tulikuwa na safari za kutazama wanyamapori asubuhi mapema, jioni na usiku. Hapa Serengeti hifadhi ni kubwa sana, tunatumia siku nzima kufanya safari za kuangalia wanyamapori,” anasema.
Mwongoza watalii, Fidelis Fabian, mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20, anasema kwa kawaida Novemba utalii hufanyika kwa kiwango kidogo, na kwamba ongezeko huwa linaanza katikati ya Desemba.
“Lakini mwaka huu, mwanzoni mwa Desemba hali ipo kama unavyoona. Maana yake wageni wamekuja na wataendelea kuja kwa wingi,” anasema Fabian kutoka Kampuni ya World Serengeti Quest ambayo ‘bookings’ zake zote zimejaa!
Kwa namna yoyote ile kuna kila dalili kuwa hadi ifikapo Desemba 31, 2025, Serengeti itakuwa imepokea wageni wengi zaidi na kukusanya fedha nyingi tofauti na miaka mingine.
Muda unaotumiwa na wageni kukaa hifadhini nao huchagiza ongezeko la mapato, na hii imetokana na ubunifu na ushirikiano mkubwa kati ya maofisa, watumishi na askari wa TANAPA, pamoja na wadau wengine wakiwamo askari polisi wa Kitengo cha Utalii na Diplomasia, na waongoza watalii chini ya TATO.
“Usalama wa wageni ndilo jukumu letu. Toka kuanzishwa kwa kitengo hiki tumekuwa msaada mkubwa kwa wageni na wengi wamekuwa wakitutumia salamu za shukrani,” anasema Mkuu wa Kitengo cha Polisi Utalii na Demokrasia, Waziri Tenga.
Afande Tenga, anasema kwa kufahamu kuwa Tanzania inapendwa sana na wageni kutoka nje ya nchini, ni muhimu kwa Watanzania kuilinda lulu hiyo kwa juhudi kubwa.
Kitengo cha Polisi UItalii na Diplomasia kimekuwa kikitoa ulinzi na msaada kwa wageni kuanzia wanapowasili viwanja vya ndege na muda wote wanapokuwa nchini.
“Mfano, mgeni akipotelewa na nyaraka zake muhimu kama pasipoti, akiripoti hapa sisi tunamsadia kupata nyaraka za muda ili aendelee na utalii na kisha arejee kwao,” anasema Afande Tenga.
Tarangire nako mambo ni moto
Kama ilivyo Serengeti, lango la kuingia Hifadhi ya Taifa Tarangire iliyopo Babati mkoani Manyara nalo limegubikwa na pilikapilika za wageni katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu.
Huko nako mapato yameongezeka kutokana na ubunifu wa wahifadhi unaowafanya wageni kutumia siku nyingi zaidi ndani ya hifadhi.
Ofisa Uhifadhi Daraja la Pili, anayeshughulikia Utalii, Calvin Lyakurwa, anasema:
“Kuanzia Oktoba mosi hadi Disemba 15, 2025 wageni ambao wameshatutembelea ni 73,372 na tumekusanya Sh bilioni 11,956,647,115.58. Hili ni ongezeko la zaidi ya Sh milioni 800.”
Marekani, Ujerumani, Uingereza, Yemen, Israel na Ufaransa ni mionghoni mwa mataifa ambayo raia wake hutembelea mara kwa mara Tarangire na hifadhi nyingine nchini.
Miongonui mwa mazao yanayotajwa kuongeza mvuto Tarangire ni utalii wa usiku na tembo wanaozaa mapacha.
“Tupo katika mchakato wa kubainisha tembo wanaozaa mapacha,” anasema Lyakurwa.
Kuhusu utalii wa usiku, anasema lengo lake ni kukabiliana na wingi wa watalii unaotokana na jitihada za serikali za kutangaza vivutio kwenye hifadhi.
Lyakurwa anasema hali ya utalii Tarangire ni nzuri na wageni wanaendelea kutembelea hifadhini hapo.
Tarangire inashika nafasi ya tatu katika kuingiza mapato kwa TANAPA ikiwa nyuma ya Serengeti na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA); lakini ikishika nafasi ya pili kwa kupokea wageni wengi nyuma ya Serengeti.
Mmoja wa watalii, Raia wa Marekani, Kelly Anderson, ni mgeni mwingine anayepaza sauti kutaja ukarimu wa Watanzania kama mioja ya vivutio vikubwa kwa wageni.
“Ninajisikia kama niko nyumbani. Kuna muunganiko fulani ukiwa Tanzania tofauti na kwingine.
“Hii ni nchi yangu ya 10 kuitembelea barani Afrika, lakini hadi sasa hapa Tarangire, ninahisi kama niko nyumbani. Ninaipenda zaidi Tanzania,” anasema.
Kelly yupo nchini kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na ameahidi kurudi tena.
Mwongoza watalii wa Kampuni ya Kilimanjaro Unforgettable, Laurent Samila, anasema utalii nchini unakua kwa kuwa wageni hupata kitu kipya wawapo Tanzania.
“Hata sisi (waongoza watalii) hatukutarajia hali ingekuwa hivi mwanzoni mwa Desemba. Tulikuwa tumekata tamaa lakini tunaona mambo yanazidi kunyanyuka. Unapewa ‘chart’ unaona kazi ni nyingi, kwa hiyo ni jambo la kumshukuru Mungu sana,” anasema Simila.
Ubora wa sekta ya utalii ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa unatokana na uwekezaji mkubwa kwenye hifadhi na uhifadhi katika utalii endelevu.
Kwa zaidi ya asilimia 30 ya ardhi yake kulindwa, nchi imeshuhudia ongezeko la asilimia 61 ya idadi ya vifaru weusi tangu mwaka 2021, pamoja na kupungua kwa asilimia 90 kwa ujangili wa tembo.
Ends