Ni takriban miaka 322 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mapadre wa Roho Mtakatifu (Holy Ghost Fathers), sasa zao jipya la shirika hilo; Shule ya Sekondari ya Wavulana Tengeru, linatimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.
Hii hapa taarifa ya ripota wa TriGen Media kutoka Tengeru, nje kidogo ya Jiji la Arusha…
Jumamosi, Oktoba 4, 2025 kunapambazuka. Kibaridi cha Arusha kinapuliza kwelikweli! Lakini hakiwazuii wageni kutoka ndani na nje ya mkoa huu kusogea mita chache kutoka Ziwa Duluti, katika bustani inayofahamika kama Tamaduni African Heritage; mali ya Tengeru Boys Secondary School and Holy Ghost Viziwi High School.

Wageni wengi wanatoka jijini Arusha na Moshi, lakini wapo wanaotokea Tengeru mjini. Sumni Joint, Tripple ‘K’ Restaurant and Lodge na Vigo Lodge ni baadhi tu ya maeneo yaliyogeuzwa nyumbani na makumi kama si mamia ya Watanzania waliokuwa na wazo moja tu; kufika Tamaduni African Heritage, Oktoba 4, 2024.
Kuna nini hasa? Kwanza ni Ibada ya Misa Takatifu inayoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Same, Ragatius Kimaryo, ikiambatana na homilia yenye mafundisho ya kuvutia; hadhari ikielekezwa kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.
Utulivu umetawala. Ukimya. Wala huwezi kujua kama wageni hao wanayafuatilia anayoyasema Baba Askofu Kimaryo! Lakini wapo. Tupo. Kipo kilichotuleta hapa pamoja. Tunakijua. Kinatuhusu. Tumedumu nacho kwa miaka minne!
Wageni wamependeza mno! Wapo ‘waliovunja’ makabati na kuibua mavazi mazuri waliyoyaficha maalumu kwa siku hiyo tu. Wapo waliovunja benki ili kufanya ‘shopping’ ya nguvu. Wapo wenzangu na mimi… lakini tupo pamoja.
Homilia inakwisha, ibada nayo inakwisha. Matangazo yanatolewa. Sauti ya MC inasikika: “…vijana wetu wahitimu watatoka nje ya eneo hili kwa ajili ya kujiandaa na kuingia rasmi ukumbini!”
Kunaanza kuchangamka. Kisa? Kauli ya MC. Vijana waliokuwa wamekaa mkabala na wageni kulia kwa ‘altare’ (baadaye inageuka kuwa ‘high table’), wananyanyuka!
Nao, kama ilivyo kwa wageni wengi, wamependeza kwelikweli! Tupo tusiojua mambo. Tusiojua ‘kupendeza’ kukoje. Tukapigwa butwaa. Tukabaki tunajiuliza: “Hivi wamevaa suti au? Vile ‘vizibao’! Aissee!” Lakini tukakiri kimoyomoyo; “wamependeza.”
Kutoka walipokuwa wamekaa hadi nje ya eneo walilopaswa kuanzia ‘maandamano’ ya kuingia ‘ukumbini’ si zaidi ya mita 50; lakini iliwachukua vijana takriban dakika 10 kufika hapo.
Ili kwenda huko, walipaswa kupita katikati ya wageni waalikwa. Hao wakashindwa kujizuia. Kila mmoja akamfuata mwanaye. Sijui ni kumpongeza au kushangaa jinsi alivyopendeza! Anajua Mungu.
Vijana hawa ndio haswa ‘wageni rasmi’ wa tukio la Oktoba 4, 2025. Wahitimu (watarajiwa) wa kidato cha nne 2025 Tengeru Boys Secondary School and Holy Ghost Viziwi High School.
Ukumbi ukachangamka, vijana wakaingia kwa mbwembwe za aina yake. Kila mwenye simu akaiinua juu kutafuta picha nzuri ya kumbukumbu. Sisi na ‘TECNO’ zetu tukawa tunaibiaibia zisionekane. Lakini tukapata picha pia.
Kuanzia hapo ikawa ni burudani kwa mwendo wa ‘bandika-bandua’. Ni kina nani waliotia fora? Jibu kila mtu analo kichwani mwake.
Wapo wanaoamini kuwa wale vijana wa ‘Msondo” ndio waliofunga kazi. Wengine tunakataa. Kwa nini wanatutania wenye vitambi? Tukakasirika. Baadhi wakaamua kuhamia kwenye ‘ofisi’ ya Mr. Mtui.
Burudani ya ‘Msondo’ na nyimbo za ‘twist’ ziliwainua vitini wageni waalikwa, wazazi na walimu. Wakajumuika stejini kusakata rhumba.
Baadaye vyeti na zawadi zikatolewa kwa wahitimu wote. Waliofanya vyema kwenye masomo wakatajwa; kwenye michezo pia; wenye nidhamu na wengine wapishi wa biriani. Ilimradi kila kijana akatambuliwa kwa kipawa alichonacho. Hii ndio Tengeru Boys.
Mambo ya kusimulia ni mengi. Mengi ya kupendeza. Kumbukumbu za kudumu. Mkurugenzi wa Shule akasimama. Padri (Jenerali) John Assey. Anataka kuzungumza neno. Shughuli inaelekea mwishoni.
Wengi tunamfahamu. Tunakumbuka mkwara aliopiga Februari 26, 2022. Visiting Day ya Kidato cha Kwanza. Ilikuwa visitation ya kwanza kwa vijana hawa wa Kidato cha IV 2025.
Leo anapiga mkwara gani? Ukumbi ukatulia. Tayari kusikiliza. Huenda leo ikawa mara ya mwisho kumsikia.
Lakini leo ni sherehe. Leo ni furaha. Kwa nini apige mkwara? Mbona ‘mapambano’ yenyewe (na kulikuwapo mapambano kweli!) yanaelekea mwishoni?
“Eti elimu yetu ni mbovu?” anaanza kusema Padri Assey. “Hawa mawaziri, maprofesa na mapadri tulionao wamesoma kwenye mfumo huu huu. Niwaulize (wazazi na wageni waalikwa), mfumo (wa elimu) ni mbovu au sisi (watu) ndio wabovu?
“Tubadilishe mfumo au tubadilishe watu? Kinachopaswa kufanywa ni kubadili watu (watendaji) na si mfumo kwa kuwa mfumo wetu wa elimu ni mfumo bora kuliko yote Afrika,” anasema.
Tukapumua. Loh! Leo anazungumzia mambo ya kitaifa? Hakuna mkwara? Hadi akamaliza. Tupo tuliodhani atasema muda wa kukaa na wahitimu ni nusu saa tu. Hapana. Hilo hakuligusa.
Padri Assey anaishauri serikali kupitia kwa Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, kutouyumbisha mfumo wa elimu, na asiiguse Elimu ya Kujitegemea (EK).
Anashangaa walimu (katika shule nyingine) kuendelea kupewa mshahara kila mwisho wa mwezi hata baada ya wanafunzi waliopita mikononi mwao kufeli mitihani kwa kupata daraja la chini kabisa; Divisheni 0.
Yote hayo yanafanyika siku ya ‘Form IV Graduation 2025’ kati ya saa mbili asubuhi na saa 11 jioni. Ni mahafali ya 18 kwa ujumla wake lakini ya tano kwa Holy Ghost Viziwi High School.
Shule mbili zilizopo Tengeru, Arusha, zinamilikiwa na Shirika la Roho Mtakatifu lililoanzishwa Mei 27, 1703 (miaka 322 iliyopita) na Padri Claude Poullart Des Places kule Rennes, Ufaransa, wakati huo akiwa na umri wa miaka 24 tu; yaani miaka minne zaidi ya umri wa sasa wa Tengeru Boys iliyoanzishwa mwaka 2005!
Angeishi leo, Padri Claude Poullart Des Places angeitwa ‘Gen Z’! Shirika hili liliingia Afrika Mashariki mwaka 1863 kupitia Zanzibar na kuweka makao Bagamoyo.
Leo limekuwa na mchango mkubwa katika sekta mbalimbali kama si zote kutokana na kutoa elimu kwa maelfu ya watu bila ubaguzi katika nchi 63 duniani; 28 kati ya hizo zikiwa barani Afrika!
Ni maono ya Padri Claude Poullart Des Places ndiyo yaliyotukusanya pale Tamaduni African Heritage Oktoba 4, 2025; pamoja na kuadhimisha miaka 20 ya shule, pia kusherehekea mchango wa shirika kwa maendeleo ya taifa na binadamu kwa jumla.
Safari ya vijana wa kidato cha nne Tengeru Boys iliyoanza Jumamosi ya Januari 8, 2022, ilifikia kilele chake Jumamosi ya Oktoba 4, 2025 huku ikitazamiwa kukamilika mwezi ujao baada ya mitihani ya taifa.
Mungu awabariki wazazi, watoto, wafanyakazi wa Tengeru Boys na wote wa shirika la Holy Ghost Fathers.