Nafasi ya ubunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi ipo wazi baada ya Kassim Majaliwa Majaliwa kutangaza kutotetea tena nafasi yake.
Taarifa kwa kina hii hapa kama inavyoripotiwa na Chriss Lilai wa TriGen Media, Ruangwa…
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza ghafla kwamba hatogombea nafasi ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Ruangwa katika Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ruangwa mchana wa leo Julai 2, 2025, Majaliwa amewashukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote akiwa Mbunge wa jimbo hilo.

“Kwa mshikamano tulioujenga, sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa Wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo kuunganisha nguvu na kusonga mbele,” anasema.
Majaliwa amekuwa Mbunge wa Ruangwa kwa miaka 15 tang mwaka 2010, kisha mwaka 2015 akateuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa Waziri Mkuu, nafasi anayoendelea kuishika hadi sasa.
Ametoa wito kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote wenye nia ya kutaka uteuzi kupitia CCM.
“Wagombea wa CCM; Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi watakapokuja, tujitokeze kwa wingi kusikiliza sera, na siku ya kupiga kura tuwapigie kura za kutosha,” anasema.
Majaliwa amemshukuru Rais Samia na viongozi wakuu wa CCM kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuwatumikia wana Ruangwa.