Home Habari za Kitaifa ‘MILANGO YA RAIS SAMIA IPO WAZI KWA MAZUNGUMZO’

‘MILANGO YA RAIS SAMIA IPO WAZI KWA MAZUNGUMZO’

0

“Milango (ya Ikulu) ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ipo wazi siku zote kwa ajili ya mazungumzo yenye malengo mema kwa mustakabali wa taifa.”

Hii hapa taarifa kutoka Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kama inavyoletwa na mwandishi wa TriGen Media

Ni kauli ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko aliyoitoa jijini Dodoma Julai 3, 2025 katika Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), alipokuwa akimwakilisha Rais Samia.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikistro Tanzania, Askofu. Dk. Fredrick Shoo akizungumza  wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) jijini Dodoma

Dk. Biteko anasema Dk. Samia hupenda kufanya kazi na viongozi wa dini kwa kuwa yeye ni kiongozi wa wananchi wenye dini mbalimbali.

 “Hata ninyi ni mashahidi. Rais amekuwa akiwaalika kuzungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa. Angekuwa ni mtu anayejifungia ndani akisema analo jeshi, sheria, katiba na vyombo vya ulinzi basi nitafanya kazi, nadhani ingekuwa ngumu sana.

“Lakini yeye amesema milango yetu iwe wazi tuzungumze na viongozi wa dini kwa ajili ya kutafuta mustakabali wa nchi yetu pale ambapo tunadhani hatuendi sawasawa,” anasema Dk. Biteko.

baadhhi ya washiriki wakifuatilia mkutano

Anasema imekuwa desturi kuwa na waangalizi wa ndani kwenye Uchaguzi Mkuu na ni imani yake kuwa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) itawaalika, akisisitiza Tume hiyo kuachwa ifanye kazi kwa uhuru.

“Tafiti zinaonesha kuwa taasisi za dini barani Afrika huchangia kati ya asilimia30 hadi 70 ya maendeleo ya sekta ya afya.

“Duniani, kwa mfano katika elimu, vyuo kama University of Edinburgh (Scotland), Oxford University (Uingereza) na University of Kwa Zulu – Natal (Afrika Kusini) vilianzishwa na taasisi za dini,” anasema Dk. Biteko.

Katika kutambua mchango wa viongozi wa dini Afrika na duniani kote, Dk. Biteko anamtaja mwanatheolojia wa Afrika Kusini, Askofu Mkuu Desmund Tutu kama kiongozi mwenye upendo, mpendahaki na amani, mtetezi wa haki za binadamu dhidi ya ubaguzi.

Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Fredrick Shoo, amemtaja Rais Samia kama kiongozi msikivu akisifu juhudi zake za kudumisha demokrasia kwa kuruhusu mikutano ya hadhara sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCT

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Askofu Dk. Shoo anasema CCT inahimiza maadili ya kisiasa na utulivu wa jamii ikiwamo kampeni safi zinazoweka mbele maslahi ya taifa na kupinga vitendo vya rushwa.

“Uchaguzi ni daraja la amani na maendeleo. Si chanzo cha mifarakano, jamii idumishe amani, mshikamano na uzalendo wa kila mmoja kwa nafasi yake. Pia INEC iendelee kusimamia haki kwa kushirikiana na waangalizi wa ndani,” anasema Askofu Shoo.

Sehemu ya wajumbe wa mkutano

 Amesema CCT itaendelea kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo ya jamii, akiiomba Serikali kutoa unafuu wa kodi na kutotoza ruzuku kwa misaada inayotolewa na wahisahi ili kuboresha huduma na kuwafikia wananchi.

Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 224 kati ya wajumbe 280.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version