Home Uchumi UPENDO WA DHATI KWA WATOTO NI ZAIDI YA ‘CHIPS KUKU’

UPENDO WA DHATI KWA WATOTO NI ZAIDI YA ‘CHIPS KUKU’

0

Chips kuku ni miongoni mwa vyakula vinavyopendwa sana hasa na watoto nchini Tanzania, kiasi cha kuchukuliwa kama ishara ya upendo pale wanapopatiwa mara kwa mara; hata hivyo, wataalamu wa uwekezaji nchini wanaamini kuwa huo si upendo wa dhati.

Fuatana na Mwandishi wa TriGen Media wa masuala ya Uchumi na Uwekezaji kwa undani wa habari hii…

Aghalabu familia za kiafrika huundwa na watu (wanafamilia) kati ya watano hadi wanane. Katika miaka ya karibuni, imekuwa kama staili kwa familia zenye uahueni wa kipato kudekeza watoto kwa namna mbalimbali, hasa kuendekeza mambo ya anasa.

“Mama sisi hatupendi ugali na maharage,” si ajabu kusikia watoto wakisema hivyo na majibu ya mzazi (baba au mama) huwa: “Nendeni mkanunue chipsi kuku.” Jamani, watoto hawataki ugali, maharage, mchicha na hata mtindi! Nini mbadala?

“Zege (chipsi na mayai) na kuku!” maelekezo ya watoto yanayotekelezwa mara moja.Kiuhalisi, kilo moja ya unga ni Sh 1,600 na hutosha kwa mlo wa familia nzima; sahani moja ya chipsi kuku ni Sh 4,000! Hiyo ni kwa ajili ya mtu mmoja tu!

Akishushia na soda ya Sh 1,000, hapo Sh 5,000 inaondoka ghafla tu!Lakini kumbe ungenunua unga wa Sh 1,600 na maji ya Sh 500 ungekuwa umeokoa Sh 2,900!.

Si hesabu ngumu hata kidogo. Ukibana au ukiokoa Sh 3,300 kwa siku; ndani ya mwezi mmoja unakuwa umeokoa takriban Sh 100,000. Pesa hiyo (Sh 100,000) ukiwekeza kwenye Mfuko wa Ukwasi (wa UTT AMIS) kwa walau asilimia 12 kwa mwaka; pesa kutoka mfukoni mwako kwa miaka 10 ni Sh 12,100,000 kujumlisha na asilimia 12 (ya riba) inakuwa zaidi ya Sh 22,000,000.

Haba na haba hujaza kibaba

Kwa hesabu hii maana yake kila siku ukitumia Sh 3,300 unapoteza Sh 22,000,000 ambayo ungeipata miaka 10 ijayo! Inatisha au inasikitisha? Jibu unalo mwenyewe. Ushauri ni kwamba, kwa kipato chochote unachopata, jaribu kuweka kiasi hata kidogo kwa ajili ya dharura.

Lipa madeni kwa mpangilio maalumu, weka kiasi hata kidogo kama akiba ya uzeeni huku ukikumbuka kuwa iko siku watoto wataenda shule au chuoni. Pamoja na ugumu uliopo, ni lazima kupambana.

Usiogope kuwaambia ukweli wanaokuzunguka kwamba huwezi kuwatimizia kila kitu; yaani chakula kama chipsi kuku, ili nao wabane tamaa na matumizi yasiyokuwa na tija.

Wanaoweza kufanya kazi, watafute hata vibarua! Hata wakati watoto wanasubiri matokeo ya mitihani (au ajira) nyakati za likizo au hata baada ya kumaliza chuo kama ilivyozoeleka, wafanye kazi fulani (kazi maana yake ajira).

Kwa sababu tatizo ni pesa na jinsi ya kuitengeneza, basi tuongelee pesa mara kwa mara katika usawa wa familia zetu. Waulize watoto au ndugu chini ya familia yako kama wana madeni na ni ya nini? Je, kila mtu ana bima ya afya?

Bima ya afya ni muhimu kwa sababu maradhi yakitokea huvuruga malengo yako kwa kuwa ni lazima kuyatibu. Kwa watoto, waambie ukweli kuhusu maisha. Waambie maisha si rahisi ila yanaweza kuwa rahisi kama watakuwa wawekezaji na kama watawekeza sehemu sahihi.

Sehemu sahihi ni wapi? Bila shaka ni katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja ya UTT AMIS. Huku, hata mwenye pesa kidogo sana ana uwezo wa kuwa mwekezaji na akawekeza mara kwa mara kadri anavyopata huku ikiwa inatoa faida jumuishi hivyo kukuza mtaji na faida yao kadri miaka inavyosonga mbele.

Ukifanya hivi utakuwa umewapa watoto wako upendo wa kweli badala ya kuwanunulia ‘chipsi mayai’.Kila mtu ni muhimu na hakuna mwenye umuhimu kama baba na mama, watoto wako nao usipime, lakini kila jambo lina mtizamo na ufumbuzi tofauti kwani usipoangalia utatuzi kwa umakini, wapendwa wako kama hawa wanaweza kuwa chanzo cha mdororo wako kiuchumi.

Kama wanakutegemea sana, kaa nao na kuangalia mpango upi utakuwa mzuri na utakuwezesha kuendelea kiuchumi vinginevyo mtakufa wote! Ondoa hisia, angalia kila jambo kiuhalisia. Tumia mifano halisi. Huo si ukatili. Ni kwa nia njema kwani uchumi wako ndiyo uchumi wao.

Wekeza kwa bidii, na ni vizuri kuanza kuwekeza ukiwa bado kijana, kumbuka kuna siri kubwa sana kati ya uwekezaji na muda, hususani pale ambapo unapata faida jumuishi kama kwenye mifuko ya UTT AMIS.

Japo thamani ya kipande (katika uwekezaji) hupanda na kushuka au inaendeana na thamani ya mifuko, bado ukianza mapema utakuwa vizuri kiuchumi miaka ya mbele.

Usisahau kuweka fungu la dharura, hilo likishapatikana, wekeza la malengo ya baadae ikiwemo kustaafu. Malengo ya kustaafu yanatakiwa yaanze siku ya kwanza unapoanza kazi. Hakika ni muhimu sana kupunguza anasa.

Lakini malengo ya baadaye si kustaafu tu, elimu kwa watoto nayo imo, fikiria wakifika chuo itakuwaje? Watoto wakifikisha miaka ambayo wanaweza kufanya kazi, wasome huku wakifanya kazi, kazi si lazima iwe ajira!

Hata nyumbani kazi zipo. Mfano, kama mnafuga kuku, ng’ombe au mbuzi, badala ya kuaajiri mtu wa kuhudumia mifugo hii, ni vizuri watoto wakapangiana zamu.

Hapo pesa ambayo ungemlipa mfanyakazi, unaiwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Kumbuka, Sh 1,000,000 ikikaa ndani ya uwekezaji kwa asilimia 15 kwa miaka 30, itakupa Sh 66,000,000!

Je, ingekuwa Sh milioni 2, 3, 4 au tano? Kama wewe ni msomi kidogo, si lazima upeleke watoto twisheni, unaweza kuwafundisha mwenyewe au kuwapa ushawishi kujiunga kwenye kundi la wale wanaofaulu vizuri darasani na kusoma pamoja.

Kwa kufanya hivyo utatengeneza fungu ambalo utaweza kuliwekeza kwenye mifuko ya UTT AMIS au kwingine.

Maofisa wa kampuni ya serikali chini ya Wizara ya Fedha, UTT AMIS, wakiwa katika moja ya mikutano

Kumbuka kuishi chini ya kipato chako, haijalishi unapata shilingi ngapi kwa mwezi, wekea walau aslimia 10 ya pesa zako na fungu la kuwekeza likiwa la kwanza kutoka katika kipato chako.

Kula kuku nusu au mzima si lazima na afya ya mwili haitaki hivyo. Kama ulikuwa unatamani kula nusu kuku, basi agiza robo!

Kama ungekula kuku mzima, basi agiza nusu. Tofauti ya unachokiagiza, kiwekeze.

Kila unapotaka kutumia bidhaa, jiulize kama nusu inatosha, pia fikiri kama ni lazima uagize zaidi ya nusu.

Ninajuwa ni vigumu kuwaambia wazazi ‘hapana!’ N pengine hata watoto. Lakini ili mipango ya pesa iwe ya uhakika inabidi uwe na uwezo wa kukataa jambo fulani ambalo usipolifanya litaleta unafuu katika maisha yako na maisha yao mbele ya safari.

Kumbuka kuwasaidia si kuwapa hela tu, nenda nao kanisani, msikitini, shambani, wasaidie katika mipango yao, watoto wape maarifa ya maisha wasiwe na akili za darasani tu.

Ugomvi na pesa kwenye familia

Tumezungumza hapo juu kuwa upendo mzuri kwa familia sio chipsi myai na kuku. Kuwekeza ndio upendo wa kweli, kwani uwekezaji utatupa pesa nyingi zaidi na pesa ndiyo kila kitu. “Pesa ni sabuni ya roho,” wanasema wahenga.

Tufanye nini sasa ili twende pamoja katika safari yetu ya uwekezaji?

Kwanza kabisa ni kupunguza ugomvi wa hela. Ni vigumu kukwepa ugomvi wa pesa kati ya mke na mume na pengine hata na ndugu ikiwemo wazazi. Ugomvi wa pesa pengine umefanya hata ndoa au familia kusambaratika.

Bajeti inaweza kuwa vita na hapa ni pale ambapo mahitaji hayawiani na kila mtu anaona hitaji lake ni muhimu zaidi ya mwenzie na pale ambapo kila mtu anapanga bajeti kivyake. Mkipanga bajeti pamoja ni kama mnawekeza pamoja sababu kila mtu anachangia na hivyo fungu la pesa za

kutumia pamoja linakuwa kubwa, pesa ikiwa nyingi unaweza fanya jambo ambalo hapo awali ulikuwa. Malengo yawe kuongeza njia za mapato, kuishi chini ya kipato, kupunguza madeni, kujifunza ili kuleta tija na kuchagua sehemu zaidi ya kutunza au kuwekeza hela zenu.

Unaweza kuwasiliana na Mwandishi wa Makala hii kwa namba +255 712 625 310

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Exit mobile version