Ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika uboreshaji wa huduma za afya nchini ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya Serikali; na hapa sekta ndogo ya afya ya kinywa na meno inamulikwa.
Kutoka jijini Dar es Salaam, hii hapa taarifa ya Florid Mapunda wa TriGen Media…
Ni ushirikiano kati ya sekta hizo ambao sasa unalenga si kuboresha tu afya ya kinywa na meno, bali kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa wepesi na kwa gharama nafuu na kuwafikia watu wengi zaidi.
Juhudi hizi zimekuwa zikifanyika katika maeneo mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu, uwekezaji katika vifaa tiba na utolewaji mafunzo kwa wataalamu.
Utafiti unaonesha kuwa takriban nusu ya Watanzania hawajahi kumuona daktari kuhusiana na matatizo au uchunguzi wa afya ya kinywa na meno.
Hali kadhalika, watoto wanne kati ya watano hawajahi kumuona daktari kuhusu suala hilo hivyo kunahitajika hamasa zaidi kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kufuatilia afya ya kinywa na meno, kama ilivyo kwa magonjwa mengine.
Katika kuhakikisha hilo, Chama cha Wataalamu wa Kinywa na Meno (Tanzania Dental Association – TDA), kiliandaa Maonesho ya Kinywa na Meno (Tanzania Dental Expo) Mlimani City jijini hapa.
Katika maonyesho hayo kulifanyika vipimo vya bure kwa wananchi kujua afya yao ya kinywa na meno, kulitolewa mafunzo kwa wataalamu wa sekta hiyo na kuonyesha vifaa vya kisasa vya matibabu ya kinywa na meno.
Pia maonyesho hayo yalilenga kuwawezesha washiriki, ambao ni wataalamu wa ndani na nje kubadilishana uzoefu na ujuzi unaoendana na ukuaji wa teknolojia.
Wadau mbalimbali wa ndani na nje, viongozi wa Serikali, madaktari, wanafunzi na wazalishaji wa dawa na vifaa tiba nao walishiriki.

Mkurugenzi wa Maonesho, Dk. Ambege Mwakatobe ambaye pia ni Mkurugenzi wa TDA, anasema ilikuwa muhimu kuwa na maonesho hayo ili kuchehemua maendeleo ya sekta hiyo ndogo nchini. Kwa muda mrefu watalaamu wa Tanzania wamekuwa wakihudhuria maonesho ya namna hiyo nje ya nchi kwa gharama kubwa.
“Hivyo tukaona sisi kama nchi tuna kila sababu ya kuandaa maonesho ya aina hii hapa hapa kwetu na kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa,” anasema Dk. Mwakatobe.
Anasema TDA wanajivunia kuona maonesho haya yakifanyika kwa mara ya kwanza nchini kwa mafanikio na kuleta hamasa ya kuendelea kuikuza sekta hiyo na kutoa huduma bora na za kisasa.
Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga, akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, anasema Serikali inatambua jitihada za sekta hiyo.
Balozi Ulanga alionesha kuridhishwa na uandaaji wa maonesho baada ya kutembelea mabanda ya maonesho.
“Tanzania inaweza kuwa kinara katika utoaji wa huduma za afya ya kinywa na meno ikiwa uwekezaji mkubwa utaendelea kufanyika.
“Kijiografia nchi yetu imekaa vizuri na itakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa nchi jirani na kuzalisha wataalamu watakaokuwa tegemeo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata nje ya jumuiya,” amesema Balozi.
Amewasifu TDA kwa kuandaa maonesho, akisema ni kielelezo tosha cha ukuaji wa sekta hiyo nchini.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Kinywa wa Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, akimwakilisha Waziri wa Fedha, amesema huu ni muda muafaka kwa wawekezaji kutumia fursa iliyopo kuanzisha viwanda vya kutengeneza vifaa tiba nchini.
“Serikali ipo tayari kupokea na kuunga mkono pendekezo lolote linaloletwa na wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta hii.
“Ndio maana hivi sasa tunaona vituo vingi vya kuoa huduma ya afya ya kinywa na meno vimeanzishwa katika miji mbalimbali nchini,” amesema Dk. Nzobo.
Anasema ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba kwa ajili ya afya ya kinywa na meno vitaleta ajira na kukuza uchumi.
Dk. Nzobo anaweka wazi kuwa ujenzi wa viwanda hivyo utasaidia kupunguza gharama za dawa zinazoagizwa kutoka nje.
Kutokana na vifaa vya kisasa vilivyooneshwa kutoka Ulaya na Marekani, anasema Tanzania tunapaswa kuwashawishi wawekezaji wajenge viwanda vitakavyozalisha bidhaa bora kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na pia wageni.
Kwa upande mwingine, Dk. Mwakatobe anasema wanafunzi na madaktari wa kinywa na meno zaidi ya 300 walishiriki maonyesho hayo huku mamia ya wananchi wakichunguzwa, kupima afya ya kinywa na meno na kupewa ushauri wa bure.
Dk. Aloyce Kabwe kutoka Mwanza ni miongoni mwa wataalamu waliohudhuria, na anasema watoto wanakabiliwa na tatizo la maradhi ya kinywa na meno kwa sababu ya kula vitu vyenye sukari.
Anaiomba Serikali isaidie kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo, kama ukosefu wa vifaa tiba vya kisasa, ambayo ni changamoto kubwa.
Boaz Nkono, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), anasema wamejifunza vitu vikubwa na kuviona vifaa vya kisasa vinavyorahisisha utendaji kazi.
Dk. Leonora Assevi amewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno kuepukana na magonjwa. “Watu wengi hawaelewi kuwa wanatakiwa kupigwa mswaki asubuhi baada ya kifungua kinywa na usiku kabla ya kulala.
“Ni vizuri wananchi wakazingatia maelekezo ya wataalamu ili kuepuka magonjwa ya kinywa na meno,” ameshauri.