Mwanasoka mashuhuri duniani, Lionel Messi, ametangaza kustaafu akiwa na umri wa miaka 38.
Hii hapa taarifa ya TriGen Media kutoka jijini Buenos Aires, Argentina…
Akizungumza na waandishi wa habari huku akibubujikwa machozi baada ya mchezo wake wa mwisho wa mashindano nyumbani dhidi ya Venezuela usiku wa jana, Septemba 4, 2025, Messi amesema:
“Huenda nikastaafu soka kabla ya michuano ya Kombe la Dunia mwakani.”

Katika mchezo huo, Messi alifunga mabao mawili wakati Argentina ikishinda mabao 3-0 katika Uwanja wa Estadio Mas Monumental, jijini Buenos Aires.
Mchezo huo wa mwisho rasmi kwake aliouita ‘maalumu sana’, ulitawaliwa na hisia za huzuni kubwa.
Messi alibubujikwa machozi mashabiki walipokuwa wakiimba na kulitaja jina lake alipokuwa akijiandaa kuingia uwanjani huku familia yake ikiwa jukwaani.
Wakati wa kutoka uwanjani, alisindikizwa na watoto wake; Thiago, Mateo na Ciro huku akiimbiwa wimbo wa taifa.
Messi anatambulika na wengi kama mchezaji bora zaidi katika historia ya soka duniani.
“Sidhani kama nitacheza mashindano yajayo ya Kombe la Dunia kutokana na umri wangu. jingine,” aliwaambia waandishi wa habari. Lakini tunakaribia na tupo pamoja. Kama nilivyosema siku zote, ninachukua siku moja baada ya nyingine huku nikitathimini afya yangu.
“Hata hivyo, bado sijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu Kombe la Dunia. Tusubiri tumalize msimu (wa ligi ya MLS 2025/26, Marekani) tuone itakavyokuwa. Itakuwa imebaki miezi sita kabla ya Kombe la Dunia.
“Mwaka huu tumekuwa na michezo mingi, msururu wa mechi. Kwa bahati, nimecheza michezo mitatu mfululizo; ni suala la siku baada ya siku. Ni wazi kwamba hii ilikuwa mechi ya mwisho ya mashindano hapa.
“Mambo mengi yametokea, na kumaliza kwa namna hii hapa ilikuwa ndoto yangu siku zote. Kuwa na nafasi ya kusherehekea na watu wangu… Kwa miaka mingi kule Barcelona (Hispania), nilikuwa nikipata upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki wa soka, na ndoto yangu ilikuwa kuupata upendo huo hapa nchini kwangu,” amesema Messi.
Mkewe, Antonela Roccuzzo, alichapisha ujumbe wa kumpongeza kupitia Instagram, akisema: “Ninajivunia sana kuwa na wewe, kila hatua unayochukua na kila kitu ulichokijenga kwa upendo na juhudi. Ni bahati iliyoje kwetu kuwa nawe kwenye safari hii! Tunakupenda.”
Kabla ya mechi, kocha mkuu wa Argentina, Lionel Scaloni, alibubujikwa machozi alipokuwa akizungumza kuhusu mchezo wa mwisho wa mashindano wa Messi kwa taifa lake.
“Huu ni mchezo ambao Leo amesema utakuwa wa kihisia, maalumu na mzuri kwa sababu ni kweli kwamba ni mchezo wetu wa mwisho wa kufuzu. Tunapaswa kuufurahia, kama tulivyokuwa tukisema siku zote,” amesema Scaloni alipozungumza na waandishi wa habari.
Argentina itakutana na Ecuador wiki ijayo, lakini Messi hatashiriki akisema kwamba, amechoka.