Tuesday, December 16, 2025
spot_img

MO AMESEMA ANACHOTOA, KLABU INAINGIZA NINI SIMBA?

Usiku wa Jumatatu iliyopita, Rais wa Heshima na Mwekezai wa klabu ya Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji aliweka wazi jumla ya pesa aliyotumia tangu 2017 hadi sasa kuwa ni Sh bilioni 87.

Fuatana na Lucy Richard wa TriGen Media katika makala haya kwa undani wa habari hii…

Mchanganuo wake ni Sh bilioni 45 za mishahara, Sh bilioni 20 ununuzi wa asilimia 49 za hisa na Sh bilioni 22 fedha za msaada wa dharura ambazo hazimo kwenye mfumo (makubaliano).

Awali, Mo aliwataka mashabiki wa Simba kujiandaa kusikia tamko lake rasmi; na kwa hakika wengi walisubiri kwa hamu kubwa ukizingatia msimu huu Simba hawakuchukua kombe lolote huku wakifungwa mara tano mfululizo na watani wao, Yanga.

Saa 4 usiku, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mo akazungumzia mambo mbalimbaki ikiwemo mabadiliko ya kikosi kwa ajili ya msimu mpya.

Kikosi cha timu ya Simba ya Dar es Salaam

Akasema watasajili wachezaji bora zaidi kwa kuwa wanapanga kufanya vizuri kimataifa; ikiwemo kubeba ubingwa wa CAF; wataunda kamati mbalimbali ndani ya Simba na kufanya mabadiliko ya Bodi ya Wakurugenzi.

Hayo yote ni ya kawaida kwani huzungumzwa kila lakini bado Simba haijakidhi kiu yake yenyewe na ya mashabiki wao, ikidaiwa kuwa hawana ‘scouting team’ nzuri ya kuwapa wachezaji bora watakaowafikisha wanapopataka.

Lakini kubwa ni juu ya fedha alizotoa yeye Mo klabuni hapo bila kuweka wazi klabu huingiza kiasi gani cha fedha kwa kila msimu; hilo sasa ndio gumzo kubwa mjini.

Wanachama na mashabiki wanataka kujua klabu yao imeingiza kiasi gani cha fedha kulinganisha na zile zilizotolewa na Mo?

Mashabiki wa timu ya Simba

Maelezo ya Mo yanaonesha wazi kuwa bila yeye Simba haiwezi kwenda kokote wala kufikia malengo yake makubwa. Bila shaka ni kweli kwamba bila pesa, huwezi kuendesha timu lakini ijulikane pia kwamba siku hizi soka ni biashara.

Kuna vitu vimejificha ndani ya Simba ambavyo viongozi hawataki kuviweka wazi.

Kwanza viongozi wanapaswa kuweka wazi suala la mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu na si Mo kuendelea kutoa pesa huku mchakato ukiwa umegota.

Habari kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba zinadai kuwa mchakato huo ulisitishwa tangu Desemba mwaka jana, kwa maana hiyo Mo hajawa mwekezaji rasmi wa Simba.

Wachezaji wa Simba Queens

Viongozi wa Simba wanapaswa kuwaeleza wanachama ni kiasi gani cha pesa kimetengenezwa na timu tangu Mo alipoingia.

Lazima pesa hizo zipo. Simba imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikifika robo fainali mara nne huku ikifika hatua hiyo mara kadhaa na hata fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hizo zote ni pesa.

Viongozi wa Simba wasema klabu imeingiza kiasi gani cha pesa kutoka kwa wadhamini wao wote tangu Sportpesa hadi sasa; zikiwemo bidhaa za Mo Dewji. Pesa hizo ziwekwe wazi kwa mashabiki na wanachama.

Waelezee mapato ya mlangoni (gate collections) ya mechi zote walizocheza ndani ya muda ambao Mo yupo na Simba ni kiasi gani.

Watueleze kwa miaka yote ambayo Mo ameingia klabuni hapo wanachama wameingiza kiasi gani kupitia ada za kila mwaka na za mauzo ya wachezaji na za jezi.

Simba wana majengo Kariakoo yanayolipiwa kodi, je kwa miaka nane ya Mo, yameingiza kiasi gani?

Mo Dewji akiwa na kocha wa Simba, Fadlu Davids

Simba wana wataalamu wazuri wa masuala ya fedha, wakae chini wapige hesabu kisha watoke hadharani kuwaambia wanachama na mashabiki na si kuelezwa upande mmoja tu; wa Mo.

Mo anasema kuna pesa anazotoa kwa ajili ya usajili, kama pesa inayotoka ni ile aliyoisema, iweje wasajiliwe wachezaji ambao hawakai Simba kwa walau misimu miwili?

Kwa nini wasajiliwe wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza kutokana na kuwa na viwango vibovu? Mo huwa anampa nani pesa za usajili halafu anamletea magalasa?

Huenda kuna watu wanampiga kwenye usajili ndio maana anatumia pesa nyingi hata katika kuvunja mikataba ya wachezaji.

Kwa nini aendelee kuwaamini wapigaji ndani ya klabu wanaomtia hasara? Je, suala hili analifurahia au lina faida kwake?

Uchunguzi wa TriGen Media umebaini kuwa kuna shida ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba inayojumuisha viongozi wote.

Hakuna uwazi kwa pande mbili kwa kuwa viongozi waliochaguliwa na wanachama wanazidiwa nguvu na wale walioteuliwa na Mo.

Baada ya vikao vya mara kwa mara vilivyofanyika hivi karibuni, viongozi (upande wa wanachama) waliomba kupewa nafasi ya kufanya hesabu wajue klabu inaingiza kiasi gani kupitia vyanzo mbalimbali tangu Mo alipoingia, ombi lililopingwa vikali.

Wachezaji wa timu ya wanawake ya Simba

“Kwa kufanya hesabu tutajua ile asilimia 51 ya wanachama imeingiza shilingi ngapi na asilimia 49 ya mwekezaji imeingiza kiasi gani.

“Pia waruhusu mkaguzi wa hesabu za serikali (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG) aingie kufanya kazi yake tujue sasa Simba inapata hasara wapi tupafanyie kazi, na kama kuna faida tujue hiyo faida inakwenda wapi na inafanya kazi gani,” anasema Mjumbe wa Bodi (jina linahifadhiwa). 

Wenye fikra pevu tumetambua kuwa Mo si kwamba amewataka wanachama wa Simba kupuuzia kutowasikiliza watu wanaodai kuwa hatoi pesa pekee, ila amewafumbua masikio wote wenye nia njema na Simba.

Yaani wanaotaka kujua kwa miaka yake minane, Simba yenyewe imeingiza jumla ya shilingi ngapi kupitia vyanzo vyake vya fedha?

Ili kuwepo usawa ni lazima pande zote mbili ziweke mbele uwazi juu ya mapato na matumizi badala ya upande mmoja pekee kufanya hivyo.

Zinazihusiana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Ungana Nasi Kupitia

0FansLike
0FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Za hivi karibuni