Changamoto ya ajira inayowakumba maelefu ya vijana wa Kitanzania, inatarajiwa kupungua kwa kiasi fulani pale kampuni ya utafiti, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa tiba itaka za afya, itakapoanza kutekeleza mpango wake mahsusi.
Mwandishi wa Joseph Mwanicheta wa TriGen Media anayo habari hii kwa undani zaidi…
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Norland, Benno Mwitumba, amesema kampuni hiyo imeanzisha mpango wa kuwawezesha vijana kupata ajira ili kupunguza wimbi la wategemezi kwa kuongeza tija kwa jamii kwa kuwa mawakala wa bidhaa zao zinazohitajika kwa wingi.
“Kuna idadi kubwa ya vijana mitaani wasiokuwa na ajira za kudumu. Sisi tuko tayari kuwapatia fursa ambapo watafanya kazi na kujilipa kulingana na bidi binafsi,” amesema.
Mwitumba amesema Norland inaleta bidhaa za kiafya ambazo zinalenga kutibu chanzo cha tatizo katika mwili wa binadamu, na kwamba bidhaa hizo zimeonesha mafanikio makubwa kwa watumiaji ndani na nje ya nchi.
“Dawa, chakula na vinywaji vinavyoingia mwilini kwa sasa vimetengeneza sumu na usugu unaosababisha miili kuwa dhaifu au tegemezi. Bidhaa zetu husaidia kurejesha afya bila kutegemea dawa nyingine za muda mrefu,” amesema.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene, alibainisha kuwa Serikali haiwezi kutoa ajira kwa kila mhitimu wa chuo kikuu kila mwaka, akahimiza sekta binafsi kushiriki katika kutoa ajira kwa vijana.
Simbachawene amewataka vijana kuchangamkia fursa za kujiajiri, hasa kupitia sekta ya kilimo na ujasiriamali, badala ya kutegemea ajira za Serikali ambazo ni chache kwa idadi.
“Kutokana na changamoto hizo zilizobainishwa na Mheshimiwa Waziri, sisi kama Norland tunatoa fursa kwa vijana wote nchini kujiunga nasi ili wauze bidhaa zetu za afya. Watapata kipato kikubwa kulingana na juhudi zao na mzunguko wa biashara wanayoifanya,” amesema Mwitumba.
Mwekezaji Mkuu wa Norland, Samuel Ikongwe, amesema huu ni wakati sahihi kwa vijana kujijenga kiuchumi kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
“Tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kupunguza tatizo la ajira nchini. Serikali inafanya kazi nzuri kwa nafasi yake, nasi kama sekta binafsi tunachukua jukumu la kusaidia wale waliokosa ajira za Serikali kwa kuwapatia fursa ya kujipatia kipato kupitia biashara ya bidhaa zetu,” amesema Ikongwe. Norland ni kampuni yenye makao makuu nchini China, na makao makuu ya kimataifa nchini Marekani. Kampuni hiyo huzalisha zaidi ya bidhaa 40 za afya, na kwa sasa ipo katika zaidi ya nchi 50 duniani kote.