Yanga Bingwa tena kwa mara nyingine,lakini katika lugha nyingine kwa Simba ya kujifariji ni kwamba kuvunjika kwa Koleo siyo mwisho wa uhunzi ndivyo tunaweza kusema.
Ni mechi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na gamu na kwa lugha ya mtaani walikuwa wakisema kuwa ina mizengwe mingi lakini hayawi hayawi yakawa.
Sasa ligi kuu ya Tanzania bara msimu huu wa mwaka 2024/25 imemalizika kwa mwendo huo,yaani kumalizika kwa mechi ya kiporo na inayoamua nani Bingwa.
Ni mechi pia iliyochezeshwa na waamuzi wa kigeni hiyo nayo ni historia nyingine mpya katika ligi ya soka Tanzania Bara.

Huu umekuwa ubingwa wa Yanga wa Nne mfululizo hawapoi hawa,lakini na wa 31 katika historia ya jumla ya Simba na Yanga katika kutwa ubingwa wa ligi kuu.
Baadhi ya wachambuzi wa soka wanasema huenda magoli yangeliweza kuwa hata zaidi ya mawili kwa kosa kosa waliokuwa nayo Yanga katika lango la Simba.Na Simba wachambuzi wanasema kuna wakati ilifika wakawa wanazuia zaidi madhara na kushambulia kwa kushitukiza baada ya kugundua kuwa hali si hali.
Hivyo hadi kipyenga cha mwisho Yanga 2,Simba Nunge. Somo la kujifunza hapa ni maandalizi lakini pia hata suala la waamuzi wa ndani imejibainisha wazi kwa namna moja ama nyingine huwa ni chanzo cha mzozo ya kisoka,kwani muamuzi wa mechi hii anadaiwa kuwa alimudu mchezo na hakuwa na mchezo dhidi ya kila aina ya maigizo.



