“Mwananchi anapotaka kuja kwako wewe kama kiongozi, asijikwae! Yaani asijiulize mara mbilimbili; niende kwa diwani au nisiende? Hivi kweli diwani atapokea simu yangu? Mwananchi anapaswa kuja kwako akiwa kifua mbele… Hata akipigia simu usiku, pokea umsikilize! Huo ndio uongozi kwa wananchi na kwa umma,” anasema William Mbogo, Diwani wa Majengo na Meya (mstaafu) wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, ambaye ameamua kung’atuka baada ya kuhudumu kama diwani kwa miaka 31.
Fuatana na Mwandishi wa TriGen Media mkoani Katavi, WALTER MGULUCHUMA, akifanya naye mazungumzo maalumu…
“Ukitaka kudumu katika uongozi kwa muda mrefu, unapaswa kufuata misingi ya uongozi bora. Kwa kiongozi wa kuchaguliwa, kampeni yako kuu ni maisha yako; yaani jinsi unavyoishi na watu.
“Maisha yako ya kila siku. Sio unakuwa mwema wakati wa kipindi cha uchaguzi tu; unashiriki misiba na kutoa misaada nyakati za uchaguzi. Unapaswa kuishi vizuri na wananchi bila ubaguzi,” anasema Mbogo kwa utulivu.

Maneno haya anayatamka wiki chache kabla ya watia nia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza kujitokeza hadharani kuchukua fomu, kama ushauri kwao huku mwenyewe akitangaza kutogombea tena udiwani.
Mbogo anafanya hivyo wakati akiwa amedumu kwenye udiwani kwa miaka 31 na kuwa miongoni mwa Watanzania wanne tu nchi nzima wenye rekodi kama yake.
Awali, Mbogo aliwaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu Kata ya Majengo mjini Mpanda kuwa ameazimia kutoendelea kuwatumikia.
“Labda kuna watakaojiuliza, kwa nini miaka 31 na si miaka 30? Awali, madiwani tulikuwa tukichaguliwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa hiyo niliingia kwenye udiwani kwa mara ya kwanza mwaka 1994,” anasema.
Anasema baada ya kipindi cha miaka mitano kumalizika mwaka 1999, utaratibu ukabadilishwa na uchaguzi wa madiwani ukaingizwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge; maana yake madiwani wa kipindi hicho waliongoza kwa miaka sita badala ya mitano.
Mbogo anaamini kwamba miongo mitatu na mwaka mmoja aliyohudumu kama Diwani, inatosha na kusema: “Sitogombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.”
Ndani ya miaka 31, Mbogo amekuwa diwani katika kata tatu tofauti ambazo ni Kabungu kwa miaka 16 (1994 – 2005); Misunkumilo miaka mitano, kisha Kata ya Majengo ambako ndiko sasa anastaafia.
“Ni muhimu sana kuwashukuru wananchi kwa kuniamini, na pia madiwani wenzangu walionipa nafasi ya kuwaongoza kama Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda 2015 hadi 2020,” anasema.
Anasema pamoja na kwamba hatogomdea uchaguzi wa mwaka huu, ataendelea kushiriki katika kazi za CCM na kuisaidia kushinda uchaguzi ujao.
Mbogo ambaye mbali na siasa, ni mkulima, mchimbaji mdogo wa dhahabu na mfanyabiashara, anakuwa mwanasiasa wa kwanza mkoani Katavi kung’atuka kwenye uongozi kwa hiari yake akiwa na nguvu; akipanga kusimamia kwa ukaribu shughuli zake binafsi.
Takwimu alizonazo, Mbogo anasema mbali na yeye, wapo madiwani wengine watatu nchini walioingia pamoja mwaka 1994 na kwamba huenda nao wakastaafu mwaka huu.
Taarifa kwamba hatogombea tena udiwani zilipoanza kusikika mitaani kabla ya yeye kuzithibitisha, kulikuwapo minong’ono kwamba anaondoka kwenye nafasi hiyo ili agombee ubunge.
Kuhusu hayo, anasema: “Niliyasikia maneno hayo. Wengine wakasema kwamba nitagombea nafasi ya juu ndani ya chama ngazi ya wilaya au mkoa. Hapana, si kweli. Nimeng’atuka na ikibidi sana labda nitagombea nafasi ya ujumbe.”
Majimbo matano ya uchaguzi mkoani Katavi ni Mpanda Mjini, Nsimbo, Tanganyika, Kavuu na Mlele na wengi wanaamini kwamba mengi kati ya hayo ‘yapo wazi’ kiushindani.
Ndani ya Kata ya Majengo, Mbogo bado anakubalika na ndio maana simanzi ilitawala alipotangaza kung’atuka. Hayo yanadhihirishwa na mkazi wa Majengo, Majaliwa Kalembo, akisema Mbogo amesimamia vyema miradi ndani ya kata akitekeleza Ilani ya Uchaguzi.
“Atakumbukwa kwa mengi kwa kuwa ameacha alama kama mnada mkubwa na kukamilika miradi ya shule za msingi.
“Alikuwa diwani msikivu kwa wananchi wanapohitaji huduma yoyte kwake. Amesaidia sana suala la ulinzi na usalama,” anasema Kalembo.Kwa upande wake, Mbogo anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi aliyoifanya yeye na Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imeusaidia Mkoa wa Katavi kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Je, ni mambo yapo ambayo hatayasahau
Anataja kipindi alipokuwa Meya wa Manispaa ya Mpanda (2015 – 2020) pale yeye na wenzake walipojikuta wakirithi kesi ya mwaka 2013.
Hilo lilitokea baada ya mzabuni kupewa Sh milioni 92 kununua gari la taka,lakini hakufanya hivyo. “Mwaka 2016 maagizo yakaja. Tukatakiwa kuwachukulia hatua za kisheria wahusika. Ikabidi wote walioshiriki kikao cha bodi wawajibike ingawa tulijua kuwa hawausiki,” anasema.
Watumishi 16 ndio waliohusika wakati walioidhinisha malipo hawazidi watu wanne na wakati huo kesi yao ilikuwa mahakamani.
Anasema ilikuwa jambo gumu kuwachanganya wote 16 na kuwachukulia hatua wakati wengi hawakuhusika.
“Hata wale waliofikishwa mahakamani, walishinda kesi! Kama tusingetumia busara, wale 16 wangefukuzwa kazi bure. Pata picha, ingekuwaje baada ya wengine kushinda kesi mahakamani?” anasema huku akihoji.