Upatikanaji wa nishati safi ya kupikia umeanza kuleta nafuu kwa wakazi wa baadhi ya maeneo ya Lindi na Pwani baada ya Serikali kupanua miundombinu ya gesi asilia majumbani, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Fuatana na taarifa ya Steven Nyamiti kutoka Pwani, kama ilivyopokewa na TriGen Media kwa undani wa habari hii…
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia ya kupikia kwa kaya takriban 1,000 katika mikoa ya Pwani na Lindi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua matumizi ya nishati safi nchini.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6 umehusisha ujenzi wa mtandao wa mabomba ya gesi wenye urefu wa kilometa 56.5 na umetekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Kupitia mradi huo, kaya 543 katika eneo la Kisemvule mkoani Pwani pamoja na kaya 470 na shule moja mkoani Lindi zimeunganishwa na miundombinu ya gesi asilia kwa matumizi ya kupikia majumbani.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mradi huo umeonyesha dhamira ya serikali ya kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira kama kuni, mkaa na mafuta ya taa.
Balile amesema hatua hiyo pia imeanza kuboresha maisha ya wananchi kwa kupunguza gharama za kupikia, kuokoa muda wa maandalizi ya chakula na kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni na mkaa.
“REA imefanya kazi kubwa kufadhili mradi huu ambao umeanza kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi. Nishati ya gesi asilia imekuwa mbadala salama na rafiki kwa mazingira,” amesema Balile wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari chini ya mwavuli wa TEF.

Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya, amesema mradi huo umefadhiliwa kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini (REF) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati safi katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Mhandisi Yessaya amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa yakichangia uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya kwa wananchi.
Mhandisi wa mradi kutoka TPDC, Anthony Karomba, amesema serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huo na hivyo amewahimiza wananchi kuilinda miundombinu ya gesi ili iweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Kisemvule wameeleza kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao kwa kuwa sasa wanaweza kupika kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi.
Wananchi hao pia wamesema matumizi ya gesi asilia yamepunguza muda uliokuwa ukitumika kutafuta kuni na mkaa, jambo ambalo limeongeza nafasi kwa wanawake kushiriki zaidi katika shughuli za kiuchumi.
Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini kama sehemu ya mkakati wa kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.



