Watoto wanaolelewa katika vituo vya malezi mara nyingi hukabiliwa na changamoto za makazi na huduma muhimu za kila siku. Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA) sasa umechukua hatua ya kusaidia kuboresha mazingira ya makazi na malezi ya watoto hao kupitia msaada wa vifaa vya ujenzi na mahitaji muhimu katika kituo cha Huruma Children’s Home jijini Dar es Salaam.
Fuatana na mwandishi wa TriGen Media kutoka Dar es Salaam kwa undani wa habari hii…
Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA) umetoa msaada wa vifaa vya ujenzi pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya kuboresha mazingira ya makazi na elimu katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Huruma Children’s Home kilichopo Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Naibu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Irine Resuile amesema msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani pamoja na utekelezaji wa sera ya taasisi hiyo ya kurudisha kwa jamii.
Irine amesema kila mwaka RITA imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za kijamii zinazolenga kusaidia makundi yenye uhitaji, ikiwemo watoto wanaolelewa katika vituo vya malezi.
Katika msaada huo, RITA imetoa vifaa vya ujenzi ikiwemo mchanga, kokoto, magodoro, vyakula pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa jengo jipya la kituo hicho.

“Watoto hawa ni kama watoto wengine tulionao majumbani na wanastahili kupata haki zao zote, ikiwemo kusaidiwa katika mahitaji yao muhimu ya kila siku,” amesema Irine.
Amesema taasisi hiyo imeendelea kuweka kipaumbele katika kusaidia watoto wenye uhitaji kwa lengo la kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kuishi na kujifunza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo cha Huruma Children’s Home Dibogo Kitang’wa ameishukuru RITA kwa msaada huo akisema utasaidia kukamilisha ujenzi wa jengo jipya litakaloongeza uwezo wa kituo hicho kupokea watoto zaidi.

Dibogo amesema kituo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa nafasi za malazi, hasa kwa watoto wa jinsia ya kiume wanaohitaji malezi na ulinzi kutoka mazingira hatarishi ya mitaani.
“Tunaendelea kupokea maombi mengi ya kupokea watoto wa kiume, lakini changamoto ya nafasi imekuwa ikituzuia kuwahudumia wote wanaohitaji msaada,” amesema Dibogo.
Amesema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kituo hicho kuongeza idadi ya watoto wanaoweza kupokelewa na kupata huduma za malezi, elimu na mahitaji mengine muhimu.

Dibogo amesema kwa sasa jengo hilo linahitaji kukamilishwa kwa kuwekwa miundombinu ya umeme na maji, pamoja na kugharamia kazi za mafundi wa ujenzi.
“Tunaishukuru sana RITA kwa msaada huu na tunaomba wadau wengine waunge mkono juhudi hizi ili kukamilisha ujenzi wa jengo hili na kuwafikia watoto wengi zaidi,” amesema.
Amesema kwa sasa watoto wanaolelewa katika kituo hicho wanaendelea vizuri na wanapata fursa ya elimu katika ngazi mbalimbali.

“Tuna watoto wanaosoma shule za awali, msingi, sekondari na hata vyuo. Tunaamini watakapokua wataweza kujiajiri au kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya taifa,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Zainab Masilamba ameipongeza RITA kwa jitihada zake za kusaidia jamii na kuhimiza taasisi nyingine kuiga mfano huo.
Zainab amesema ushiriki wa taasisi na makampuni katika kusaidia makundi yenye uhitaji ni muhimu katika kujenga jamii yenye mshikamano na ustawi kwa wote.



