Monday, April 13, 2026
spot_img

EACOP yazindua mpango wa ‘Msaidie Binti Abaki Shule’

Katika maeneo mengi ya vijijini, changamoto ya hedhi ni sababu inayowafanya baadhi ya wasichana kukosa masomo kila mwezi. Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) sasa umeanzisha mpango maalumu unaolenga kusaidia kubadilisha hali hiyo kwa kuwapatia wasichana elimu na mahitaji muhimu ya hedhi salama ili waendelee na masomo bila vikwazo.

Fuatana na mwandishi wa TriGen Media kutoka Singida kwa undani wa habari hii…

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umeanzisha awamu ya kwanza ya mpango wa hedhi salama mashuleni unaojulikana kama “Msaidie Binti Abaki Shule”, unaolenga kuwawezesha wasichana hususan wanaoishi vijijini kuhudhuria masomo muda wote shuleni na kuongeza ufaulu wao darasani.

Meneja wa Uwezeshaji na Uwajibikaji kwa Jamii wa EACOP, Clare Haule, amesema mpango huo umeanza kutekelezwa katika mikoa ya Singida, Shinyanga na Dodoma, ukihusisha jumla ya shule 19 na kunufaisha zaidi ya wanafunzi 4,596.

Amesema katika awamu ya kwanza mpango huo umeanza katika shule sita mkoani Singida, saba mkoani Shinyanga na sita mkoani Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Singida, Chistopher Kidubo, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa ‘Msaidie Binti Abaki Shule’ unaoratibiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)

“Mpango huu umeanza kwa awamu, na katika hatua ya kwanza tumelenga mikoa hiyo mitatu kabla ya kuendelea na maeneo mengine nchini. Kwa ujumla tunatarajia kuwafikia wanafunzi 4,596 katika shule 19,” amesema Clare.

EACOP imeanzisha mpango huo kama sehemu ya mkakati wake wa uwekezaji na uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwa wananchi wanaoishi katika maeneo unapopita mradi huo katika mikoa nane nchini.

Amesema tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 15 hadi 20 ya wasichana hukosa masomo kwa siku moja hadi mbili kila mwezi kutokana na hedhi, hali inayotokana na ukosefu wa taulo za kike na mazingira salama ya kujistiri shuleni.

Kupitia mpango huo, EACOP imeanza kutoa elimu ya afya ya uzazi, taulo za kike na uhamasishaji wa hedhi salama ili kupunguza changamoto ya utoro na ufaulu hafifu miongoni mwa wanafunzi wa kike.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Victorina Ludovick, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi, amesema mpango huo unaendana na malengo ya Dira 2050 inayosisitiza usawa wa kijinsia na upatikanaji wa mahitaji muhimu kwa watoto.

“Kwa kusaidia usimamizi wa afya ya hedhi salama shuleni tunajenga msingi wa wanawake bora na wenye uwajibikaji kwa taifa letu,” amesema Dk. Victorina.

Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Regina Yaghambe, amesema mpango huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa utasaidia kupunguza utoro miongoni mwa wasichana unaosababishwa na ukosefu wa mazingira salama ya hedhi shuleni.

Baadhi ya wazazi waliohudhuria uzinduzi huo wamesema kabla ya mpango huo watoto wao wamekuwa wakikosa masomo wanapokuwa katika hedhi kutokana na ukosefu wa taulo za kike na sehemu salama za kujistiri.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Victorina Ludovick, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego .

Wamesema wakati mwingine wamekuwa wakilazimika kuwapatia watoto wao vipande vya nguo au hata majani ya mimea kujisitiri kutokana na ukosefu wa taulo za kike, hasa katika maeneo ya vijijini.

“Tunaishukuru EACOP kwa kuanzisha mpango huu kwa ajili ya wasichana wetu. Huu ni msaada mkubwa unaowasaidia kujiamini na kuendelea na masomo yao,” amesema Faulina Sinde, mkazi wa Igauli.

Wanafunzi waliopokea msaada wamesema taulo hizo zitawasaidia kuhudhuria vipindi vyote vya masomo bila kukosa kama ilivyokuwa hapo awali.

Mmoja wa wanafunzi hao, Edina Metusaeli, anayesoma kidato cha nne Shule ya Sekondari Ntonge, amesema msaada huo umewaongezea kujiamini wanapokuwa katika hedhi.

“Taulo hizi zitatusaidia kuhudhuria vipindi vyote na kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zetu,” amesema.

Uzinduzi wa mpango huo umefanyika katika Shule ya Sekondari Igauli iliyopo katika Kijiji cha Igauli, Kata ya Ntonge, Halmashauri ya Wilaya ya Singida.

Mradi wa EACOP wenye urefu wa kilomita 1,443 unaanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga nchini Tanzania.

Wanahisa wa mradi huo ni TotalEnergies (asilimia 62), TPDC (asilimia 15), UNOC (asilimia 15) na CNOOC (asilimia 8).

Zinazihusiana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Ungana Nasi Kupitia

0FansLike
0FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Za hivi karibuni