Balozi Stephen Patrick Mbundi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hii hapa taarifa fupi iliyoifikia TriGen Media kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki…
Balozi Stephen Patrick Mbundi ni mwanadiplomasia mwandamizi wa Tanzania na kiongozi wa serikali mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 28 katika utumishi wa umma.
Kabla ya uteuzi wake kuwa Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Mbundi alihudumu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akisimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akiwa Katibu Mkuu, Balozi Mbundi alichukua nafasi muhimu katika kupanga na kusimamia sera za mahusiano ya kimataifa ya Tanzania, hususan katika masuala yanayohusu ushirikiano na mchakato wa ujumuishaji wa kikanda ndani ya EAC. Aidha, mara nyingi aliwakilisha Tanzania katika mikutano mbalimbali ya ngazi za juu ya kimataifa na kikanda.

Katika kipindi chake cha utumishi, Balozi Mbundi amefanya kazi kwa karibu na vyombo na taasisi mbalimbali za EAC, washirika wa maendeleo pamoja na taasisi za sekta binafsi kwa lengo la kuendeleza ajenda ya ujumuishaji wa kikanda.
Vilevile, ameshiriki katika majadiliano na viongozi na wataalamu kutoka nchi wanachama wa EAC ili kutafuta suluhisho la changamoto zinazokwamisha uhuru wa biashara na usafiri wa watu ndani ya Jumuiya hiyo.
Kwa uzoefu wake wa muda mrefu katika masuala ya ujumuishaji wa Afrika Mashariki, uteuzi wa Balozi Mbundi unatarajiwa kuleta msukumo mpya katika kuimarisha ushirikiano na maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.



