Monday, April 13, 2026
spot_img

Serikali yapanga kumaliza changamoto ya usafiri Dar

Usafiri wa umma, miongoni mwa huduma muhimu mijini, imekuwa na changamoto nyingi hususan kwa Dar es Salaam; jiji lenye wakazi wengi zaidi nchini, na sasa Serikali inajipanga kuchukua hatua stahiki.

Fuatana na mwandishi wa TriGen Media aliyepo jijini Dar es Salaam kwa undani wa taarifa hii.

Ni mikakati inayolenga kuwapatia maelfu kama si mamilioni ya wakazi wa Dar es Salaam huduma bora, ya haraka na yenye uhakika ya usafiri.

Akizungumza jijini hapa baada ya Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kufanya ziara kukagua miundombinu ya usafirishaji, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati, Dk. Jim Yonazi, amesema serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kuboresha sekta ya usafiri wa umma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Dk. Jim Yonazi (wa pili kushoto) akikagua kituop cha Ubungo Terminal

Amesema katika ziara hiyo kamati imetembelea Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) pamoja na Kampuni ya Uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) na kujionea maendeleo ya uwekezaji uliofanywa.

“Ni dhamira ya serikali kuhakikisha usafiri wa Dar es Salaam unakuwa bora, wa kisasa na unaokidhi mahitaji ya wananchi. Tumejionea miundombinu iliyowekwa na jitihada zinazoendelea kuboresha huduma,” amesema Dk. Yonazi.

Amebainisha kuwa tayari kampuni zimeanza kuleta mabasi mapya, hatua itakayoliwezesha jiji hilo kuwa miongoni mwa majiji yenye usafiri wa kisasa barani Afrika.

Dk. Jim Yonazi akikagua moja kati ya vituo vya BRT Phase II, Barabara ya Kilwa

Aidha, amesema mabasi mengi yanatarajiwa kutumia gesi asilia, huku serikali ikiwa imejenga miundombinu ya vituo vya gesi ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi.

Kwa upande wa teknolojia, Dk. Yonazi amesema serikali imewekeza katika mifumo ya TEHAMA itakayomwezesha mwananchi kutumia kadi maalumu kulipia nauli bila kulazimika kupanga foleni, jambo litakaloongeza ufanisi na kupunguza usumbufu.

Katika hatua nyingine, amewahakikishia wananchi kuwa mabasi yote yaliyoharibika yanafanyiwa ukarabati ili yarudi barabarani na kuimarisha upatikanaji wa huduma.

Dk. Yanazi akipata maelezo kuhusu kadi za kusafiria za DART

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, Said Tunda, amesema lengo kuu ni kurejesha furaha kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa kuwapatia usafiri wa uhakika.

Pia amewataka waendesha daladala kuendelea kutoa huduma huku serikali ikiendelea kufanya mazungumzo nao ili kupata utaratibu bora wa ushirikiano, hususan kwa zile zilizopewa kibali cha kutumia barabara ya mwendokasi.

Hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha maisha ya wananchi kupitia miundombinu imara na huduma bora za kijamii.

Zinazihusiana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Ungana Nasi Kupitia

0FansLike
0FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Za hivi karibuni