Ni mkakati au kampeni inayofahamiak kama ‘Kila Mtu Atibiwe Kwao’ inayoendelea kushika kasi katika Jimbo la Kisarawe ikiambatana na juhudi za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Pata taaarifa hii kwa undani zaidi kutoka kwa mwandishi wa TriGen Media aliyepo Kisarawe mkoani Pwani.
Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Kola, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dk. Selemani Jafo, amesema anaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha kila kijiji kinapata zahanati ili kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Katika muendelezo wa kampeni hiyo, Dk. Jafo amechangia tofali 1,500 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya itakayohudumia wakazi wa eneo hilo.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya vijijini, hususan kwa wajawazito, watoto na wazee ambao mara nyingi hukumbana na changamoto ya kufuata matibabu mbali na makazi yao.

Dk. Jafo amesisitiza kuwa kampeni ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao” inalenga kukamilisha ujenzi wa zahanati katika kila kijiji ndani ya Jimbo la Kisarawe, akibainisha kuwa huduma za afya ni haki ya msingi kwa kila mwananchi.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinaendeleza mafanikio aliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, ambapo aliweza kuhamasisha ujenzi wa zahanati 27 kupitia ushirikiano wa Mfuko wa Jimbo, Halmashauri, Serikali Kuu pamoja na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masaki, Pili Chamgui, amempongeza Dk. Jafo kwa juhudi zake za dhati katika kuwajali wananchi, akisema kwa sasa vijiji vyote vya kata hiyo vina zahanati pamoja na Kituo cha Afya cha Masaki kinachotoa huduma za upasuaji.
Amesema ujenzi wa zahanati katika Kitongoji cha Kola unakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo ambalo liko mbali na kijiji mama cha Kisanga, hali iliyokuwa ikiwalazimu wakazi kusafiri zaidi ya kilometa sita kufuata huduma za afya.
Nao wananchi wa Kitongoji cha Kola wameeleza shukrani zao kwa mbunge huyo wakisema amesikia kilio chao cha muda mrefu cha ukosefu wa huduma za afya karibu na makazi yao, jambo lililokuwa likiwaweka katika hatari hasa wakati wa dharura za kiafya.
Kampeni ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao” inaendelea kuleta matumaini mapya kwa wananchi wa Kisarawe, huku ushirikiano wa viongozi na jamii ukiendelea kuwa chachu muhimu ya kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.



