Haki za watoto wenye ulemavu jijini Arusha zinavunjwa kwa kuwafanya nyenzo ya kuombaomba mitaani.
Fuatana na Egidia Vedasto wa TriGen Media kwa undani wa habari hii ya kusisimua…
Kuna mtu nyuma ya biashara ya watoto ombaomba jijini Arusha anayedaiwa kuwafadhili.
Taarifa zinasema kwamba mfadhili huyo huwatoa mikoani na kuwaleta jijini, kisha kuwapatia malazi, viti mwendo na kuwatumia wazazi wa watoto hao ‘mshahara’ (posho) kila mwisho wa mwezi.
Ulemavu hutokana na dosari ama mwilini au akilini zinazosababisha mtu kushindwa kutenda mambo ambayo kwa kawaida angetarajiwa kuyaweza, hivyo kuwa kizuizi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Hata hivuo, mlemavu yeyote anastahili au aha haki ya kupata huduma zote za kijamii kama afya, elimu na mazoezi inapowezekana kumsaidia kufikia malengo yake ya maisha.
TriGen Media imezungumza na baadhi ya watoto wenye ulemavu waliopo jijini Arusha na kubaini kuwa wengi miongoni mwao hutokea mikoa ya Kanda ya Ziwa; Simiyu, Shinyanga na Mwanza.
Watoto hao wanaonekana kufurahia maisha ya mjini yanayowapatia pesa kwa urahisi tofauti na vijijini walikokuwa wakitegemea zaidi kilimo, huku pia kukiwepo dhana potofu kwamba ulemavu ni mkosi katika familia.
Hata hivyo, imegundulika kuwa licha ya watoto hao kufanya kazi katika mazingira magumu ya jua na mvua, anayefaidi zaidi ni mfadhili wao na msaidizi wake; yule anayemsukuma mlemavu husika kwenye kiti mwendo.
Kijana Antony (si jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 17 ambaye kazi yake ni kusukuma kiti mwendo cha mtoto mwingine mwenye umri wa miaka 13 asiyeweza kuzungumza wala kusimama, anasema:
“Kwetu ni Simiyu, huyu ni mdogo wangu, mama yetu anaishi Lamadi. Hapa Arusha tunaishi mjini kati, eneo hilo kuna walemavu wengi tu.”

Wakati wa mazungumzo hayo Anthony alionekana wazi akiwa na hofu na kutotaka mwandishi wa makala haya afahamu eneo hasa anakoishi.
Inaaminika kuwa wengi wanaosaida kuwasukuma walemavu huwa si ndugu zao wa damu, kitu kinachotia shaka juu ya usalama wao dhidi ya ukatili wa kingono.
Kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma, lakini utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) unaonesha kuwa kati ya watoto milioni 240 wenye ulemavu duniani, nusu hawajawahi kuhudhuria shule, theluthi moja hawapati chakula bora na cha kutosha na wanawakilishwa kwa njia isiyo sawa. Wengi wao wanaachwa nyuma.
UNICEF inadhamiria kuhakikishia kuna ujumuishaji wa watoto wote wenye ulemavu katika elimu, afya, majibu ya dharura, ulinzi wa kijamii, familia na maisha ya jamii.
Katika Mkutano wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu 2022, UNICEF imejitolea kutoa ushahidi mpya kupitia utafiti, kuanzisha ajenda ya utafiti wa kimataifa na jukwaa kwa watoto wenye ulemavu ili kuhakikisha wanajumuisha ulemavu katika tafiti zote na kuongeza uwekezaji katika ujumuishaji kwa watoto.
Mashuhuda wazungumza
Mmoja wa watu wenye ulemavu ambaye hakutaka kutaja jina lake aliyekutwa Soko la Kilombero jijini Arusha, anasema:
“Mimi nimeolewa, nina watoto wawili. Kabla ya kuja Arusha nilikuwa nikiishi na mume wangu, lakini jamii ilinidhihaki na kunibeza, walikuwa wakimuuliza mume wangu ameoaje mwanamke wa aina hii?
“Tangu nimekuja hapa ninashukuru maana hakuna mtu anyemwangalia mwenzake. Hapa kila mmoja anafanya shughuli zake na ninafurahia maisha kwani nakula vizuri, nalea watoto wangu na kutuma pesa za shamba kwa mume wangu.”

Anasema kwa upande wao watu wazima wenye ulemavu, hakuna changamoto kwa sababu wanajitambua, lakini watoto wadogo hukumbana na changamoto hasa kudhulumiwa fedha, kukosa watu wa kuwahudumia chakula na usafi pamoja na kukosa uangalizi.
Anasema watoto hao huchukuliwa kutoka vijijini kwa wazazi wao na kuja mjini kutumikishwa kama ombaomba.
“Siwezi kujua nani anawachukua kutoka huko hasa Kanda ya Ziwa. Wazazi wao hutumiwa kati ya Sh 50,000 hadi Sh 100,000 kila mwezi huku watoto wao wakihifadhiwa katika nyumba za kulala wageni. Wengine kupangishiwa vyumba na kupewa viti mwendo.
“Si unajua Wasukuma hujishughulisha sana na kilimo? Sasa mzazi anaona mtoto hatembei na hajiwezi kwa chochote, inakuwa ni usumbufu maana hawezi kufanya kazi zake kwa uhuru, hivyo anaona bora mtoto aondoke tu, yeye abaki huru na apate hiyo posho ya kila mwezi.
“Unamwona yule mtoto pale (anaonyesha kwa kidole)? Miaka yake haifiki 12, cha kushangaza wazazi wake hawapo hapa Arusha, wapo kijijini wanasubiri mwisho wa mwezi walipwe kupitia yeye.
“Hii ni hatari kwa sababu akifanyiwa vitendo vibaya hana wa kumsaidia, bora yetu sisi watu wazima tunaweza kujipambania ma kusema ndiyo au hapana,” anasema.
Uchunguzi wa TriGen Media umengudua kuwa idadi kubwa ya ombaomba jijini Arusha wanaishi Kata ya Unga Limited ambako wanafadhiliwa na mtu asiyejulikana.
Ni jukumu la serikali kumbaini na kukomesha uovu huo.

Mwaka jana, gazeti la uchunguzi la JAMHURI liliandika ripoti kuhusu utumikishwaji wa kingono kwa watoto ombaomba jijini hapa, lakini hadi leo hakuna hatua stahiki iliyochukuliwa huku hali ikizidi kuwa mbaya na kuchafua taswira nzuri ya jiji la kitalii la Arusha.
Baadhi ya watoto waliohojiwa kuhusu uwepo wa vitendo vya ukatili wa kingono, wamekana na kudai kuwa hata kama vipo basi vinafanyika kwa makubaliano.
Akizungumza na TriGen Media, Mwanasheria Richard Manyota amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto kifungu namba 16 ya mwaka 2014, ni kosa kisheria kwa wazazi (baba, mama au mlezi) kutomlea mtoto.
“Mtoto huangaliwa kwa mujibu wa sheria, na kwa maslahi mapana bila kujali uwezo wa kifedha,” anasema Manyota.
Anamtaja Ofisa Ustawi wa Jamiii kuwa ndiye mwenye jukumu la kwenda mahakama ya watoto na kufungua maombi maalumu ili mahakama imuamrishe mzazi au mlezi kutekeleza majukumu ya malezi kwa mtoto.
“Asipowajibika, basi Ofisa Ustawi wa Jamii ataiomba Mahakama itoe amri ya kumwondoa mtoto mikononi mwa mzazi au mlezi na kumpeleka katika taasisi maalum ya malezi.
“Kwa sasa kuna wimbi kubwa la watoto walemavu wenye umri kati ya miaka minne hadi 15 kukaa kando ya barabara au wakitembea katikati ya barabara wakiombaomba; wengine wakitembezwa kwenye vitimwendo na wengine wakiwatembeza watu wazima.

“Sheria ipo wazi, ni kosa la jinai la sheria ya usalama barabarani, maana sheria inamtambua askari wa usalama barabarani pekee, kuwa ndiye anayeweza kusimama (au kutembea) katikati ya barabara akiongoza magari, hivyo watoto hao wanapaswa kuondolewa kwa sababu ni kosa na hatari Kwa usalama wao.
“Ni ngumu kumshitaki mtoto kwa kosa la kusimama na kuomba pesa barabarani, kuna taarifa kwamba kuna watu wanaowatumia ili wajinufaishe, inasadikika kwamba wanahifadhiwa Kata za Sekei, Ngarenaro, Unga Limited na maeneo mengine ya Arusha.
“Juni mwaka jana kulikuwa na kesi Mahakama Kuu, Mahakama iliwafunga miaka saba jela watu watatu, wanawake wawili na mwanaume mmoja na kuwaamuru kulipa faini ya Sh 5,000,000 kila mmoja watakapomaliza kutumikia kifungo.
“Wawili kati yao walikuwa wakitokea Mwanza na mwanamke mmoja alitokea Arusha ambaye alifanya kazi ya kuwatafutia vyumba vya kuishi watoto ombaomba.
“Watu hao walikuwa wanawalaghai watoto kwamba watawapeleka shule, lakini baada ya kuwafikisha mjini waliwaambia wajifanye walemavu na kuanza kazi ya ombaomba ili wajinufaishe, watoto waliotoa ushahidi na kuwafichua wahalifu, walionekana vipofu na wengine walemavu, kumbe siyo kweli,” anasema Wakili Manyota.
Anasema Sheria ya Mtoto inawataja askari polisi, wazazi na maofisa ustawi wa jamii kuangalia suala la mtoto kwa mustakabali wa maisha yao, na iwapo watoto watakamatwa na kupelekwa polisi bila kufikishwa mahakamani kunakosekana nguvu ya sheria kwa ofisa ustawi wa jamii kufanya kazi yake kwa usahihi.
Naomi Kimaro ofisa wa kituo cha kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, Amani Centre, anakiri kuongezeka kwa watoto ombaomba wenye ulemavu jijini Arusha.
“Hii naiona kama sababu ya kuchangia kudorora kwa elimu kwa mtoto. Mfano, suala jingine ni pale mtoto akitoka na mzazi au mlezi ambaye ni mlemavu, mzazi anamtumia mtoto kama kiongozi wake wakiwa barabarani, hivyo ni lazima ashinde naye kutwa nzima, hivyo ni ngumu mtoto huyo kupata haki yake ya elimu.
“Shirika letu tuna maofisa ustawi wa jamii, wanaofuatilia mitaani usiku na mchana kubaini watoto wanaoishi mazingira magumu, ambapo wakipatikana tunatafuta familia zao ili kujua shida ipo wapi, baada ya hapo tunahakikisha kama mtoto aliyeacha shule anarudishwa au kuanza masomo ya elimu ya watu wazima kama hajawahi kwenda shule,” anasema Naomi.
Anashauri serikali iweke sera mahsusi za namna ya kukomesha utumikishwaji wa watoto wenye ulemavu, jamii kutumia njia za uzazi wa mpango ili kupanga idadi ya watoto watakaoweza kuwalea.
Pia amewashauri wazazi kuzungumza na watoto na kuwalea katika misingi bora bila kujali hali ya mtoto wake, pia serikali kuziunganisha kaya zenye watoto wenye ulemavu na TASAF ili kuwasaidia wazazi hao kuhudumia familia zao.
“Mwaka jana tuliletewa mabinti wawili wenye ulemavu, baada ya kuwapokea tuliwasiliana na ofisa ustawi wa jamii awasiliane na mwenzake eneo walikotokea, Kanda ya Ziwa.

“Baada ya kuwajulisha kuwa kituo chetu hakihudumii watoto wenye ulemavu, walianza kufanya mazoezi ya kutembea na hatimaye walitembea vizuri, ndipo tukagundua kuwa hawana ulemavu licha ya kwamba walifikishwa ofisini kwetu wakiwa na viti mwendo, hii ilitupa picha kuwa, wengi wanajifanya walemavu ili wapate pesa lakini sio walemavu” anasema Naomi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Amon Mpanju, anasema utumikishwaji wa watoto wenye ulemavu haukubaliki kwa kuwa ni kinyume cha Sheria Namba 9 ya mwaka 2010, kunakinzana na sheria za nchi.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakataza utumikishwaji wa namna yoyote ile ambao unalenga kumbagua au kumnyanyapaa mtu, na sheria ya mtoto inazuia utumikishwaji kwa lengo la mtu kujiingizia kipato na ni kosa la jinai, mtoto akiwa na ulemavu isiwe sababu ya kugeuzwa kitega uchumi,” anasema Mpanju.
Mpanju anasema suala hilo ni vema lizungumziwe na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwa ndiyo wenye ufafanuzi na mikakati ya kupambana nalo, kwamba amelizungumzia kidogo kwa sababu limehusisha watoto.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Denis Mgiye anasema kuna zaidi ya watu 120 wanaokaa kando ya barabara katikati ya Jiji la Arusha wakiombaomba, hususan Philips, Mianzini na Sanawari katika barabara ya Arusha – Moshi.

“Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kilitoa maelekezo ya kufanyika ‘operesheni rafiki’ ya siku tatu Aprili mwaka huu na kufanikiwa kukamata ombaomba zaidi ya 40, miongoni mwao wapo wanaoigiza ulemavu. Operesheni hiyo itakuwa endelevu kwa kushirikiana na mgambo wa jiji hadi changamoto hiyo iishe.
“Wito wangu kwa jamii, mtu akitaka kutoa sadaka yake namshauri aipeleke kanisani, msikitini au apeleke ofisi za ustawi wa jamii, tukiendelea kuwapa tunachochea ongezeko lao.
“Ukiongea nao wengi wanaonyesha kupata pesa sana hata zaidi ya watumishi wa umma na ukichunguza kwa nini wengi wanakuja Arusha utaambiwa kuwa watu wa huku ni watoaji (wakarimu) sana kuliko mikoa mingine,” anasema.
Anasema ni makosa kisheria kwa mtu yeyote kujihusisha na shughuli za kuombaomba au kumtumia mtu kuomba kwa ajili ya kujiingizia kipato. Wilaya zenye tatizo hili ni Meru, Arusha Jiji na Arusha DC.
“Serikali imetenga fedha kwa ajili ya watu wenye ulemavu; asilimia mbili ya mapato ya halmashauri, mkopo usiokuwa na riba, lakini kutokana na pesa wanazopata barabarani kuwa nyingi, wanakwepa kuungana katika vikundi ili wakopeshwe na kufanya shughuli za ujasiriamali,” anasema.
Diwani wa Unga Limited aliyemaliza muda wake ambaye anagombea tena nafasi hiyo, Mahmoud Said Omary, anasema Baraza la Madiwani liliweka mikakati ya kuzitaka idara zinazohusika na ustawi wa jamii kushughulikia suala hilo.
Anasema watu wenye ulemavu wanaofanya shughuli za kuomba jijini humo wanaishi mazingira magumu hasa kipindi cha mvua kutokana na tishio la kupata magonjwa ya kifua na yale ya kuambukiza.
“Ni kweli kuwa kuna mtu nyuma ya kundi la watoto na watu wazima wenye ulemavu wanaofanya shughuli za kuombaomba, lakini naamini kwa mkakati huu uliowekwa tatizo hili litapata ufumbuzi na ninashauri jitihada zisifanywe na wilaya wala mkoa, bali ziwe za kitaifa, ili tuweze kuondokana na vitendo hivyo.
“Ukweli watoto wenye ulemavu wanatumikishwa na wanateseka sana, kwa mfano kipindi cha mvua mtoto anaamshwa usiku kuwahi magari ya kwenda Moshi mjini au Soko la Sadala wilayani Hai wakaombe, unakuta mvua na baridi vinamwishia mwilini, wakati huo mzazi yupo mkoani anasubiri ujira wake. Matokeo yake anayenufaika ni mtu aliyepo nyuma ya mtoto kwa maana aliyemchukua kutoka kijijini,” anasema Mahmoud.
Kuhusu mazingira wanayoishi, anasema watoto huwekwa wengi kwenye chumba kimoja, huku wakilalia na kujifunika turubai na kwamba awenye bahati ya kupata godoro, godoro moja hulaliawa na kati ya watu wanane hadi 10 hali inayohatarisha usalama wa afya, vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti.
“Ikumbukwe watu wanaotumikisha watu wenye ulemavu wana pesa sana, wana mtandao mkubwa. Ukienda Zanzibar wamejaa, na sasa wamefika Mombasa, hali hii inachafua taswira ya nchi yetu, nashauri uwekwe mkakati wa kitaifa wa kumaliza ombaomba mitaani,” anasema.



                                    