Wakati macho na masikio ya mamilioniya Watanzania yakielekezwa jijini Dodoma, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu wanadai kuwapo kwa rafu katika vikao vya chini vya uteuzi wa wagombea ubunge.
Fuatana na Mwandishi wa TriGen Media mkoani Shinyanga kwa undani wa habari hii…
Makada watatu wa CCM wa Kishapu mkoani Shinyanga wanadai kwamba mmoja wa watia nia wa nafasi ya ubunge, Lucy Mayenga, amedanganya katika kujaza fomu za maadili.
Wakizungumza na mwandishi wa TriGen Media, makada hao wanasema wamemwandikia barua Katibu wa CCM wilayani humo kupinga kuwamo kwa jina la Lucy miongoni mwa wagombea, wakidai kuwa amewahi kushitakiwa na kuhukumiwa mahakamani.
Barua ya Julai 4 mwaka huu kwenda kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kishapu (nakala tunayo), inasomeka:
“Tunapenda kukutaarifu kuwa mgombea ubunge Kishapu ana kesi na alishahukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Februari 14, 2023.”

Barua hiyo iliyosainiwa na Michael Jagadi Masanja, John Katambi Jibusa na Jinamabi Pastory inassema kesi inayomuhusu Lucy ni ya madai Namba 20 ya mwaka 2021.
“Kimaadili si sahihi kumteua mgombea wa namna hii kwa sababu chama kinaweza kupoteza jimbo na kuwaumiza wanachama wa CCM wa KIshapu,” inasema barua hiyo.
Mmoja wa makada wa CCM aliyesaini barua hiyo ameiambia TriGen Media kuwa nakala ya hukumu dhidi ya Lucy ipo wazi, lakini katika fomu ya maadili ya chama, amesema kuwa hajawahi kushitakiwa.
Nakala ya hukumu hiyo iliyosainiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Athuman Matuma, inaonyesha kuwa mlalamikaji katika shauli hilo alikuwa Kampuni ya Gat Engineering dhidi ya Lucy na Cassian Fidelis.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, amewataka makada hao na wanachama wengine kuwa wavumilivu kwa kuwa muda wa kuweka pingamizi kwa wagombea bado upo.
“Vikao vinavyofanyika ni vya siri, sasa wao wamejuaje kama amepitishwa? Mnapaswa kujiridhisha kwanza kabla ya kuandika kwa kuwa siku majina yatakapotangazwa na kukuta jina la mgombea huyo halipo, itakuwa aibu kwenu,” anasema Odilia bila kuweka wazi iwapo ameipata barua ya malalamiko hayo.
Baadaye, mwandishi wa habari hii alimtafuta Lucy Mayenga kutaka kujua ukweli kuhusu malalamiko dhidi yake.
Baada ya kujitambulisha na kuzungumza hili na lile, mwandishi akataka kujua iwapo katika fomu ya maadili, Lucy alikana kuwahi kuwa na kesi ya madai.
Swali hilo halikujibiwa kwani Lucy alikata simu, na alipopgiwa tena, akajibu: “Niko barabarani kijijini, nitakutafuta nikifika.”
Hata hivyo, Lucy, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, hakupiga tena simu kama alivyoahidi.
Kipengele cha ‘tabia na maadili’ katika fomu ya kugombea ndani ya CCM kinamtaka mtia nia au mgombea kueleza iwapo amewahi kupatikana na hatia katika kosa lolote la jinai au madai mbele ya vyombo vya dola vya kutoa haki.



