Soka, mmoja kati ya michezo inayopendwa zaidi duniani, imepitia milima na mabonde ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rangi wa hali ya juu; ambapo watu weusi, wengi wakiwa na asili ya Afrika, wakiwa waathirika wakubwa kwa imani kwamba hawana uwezo. Hata hivyo, wapo waliojitosa na kuthibitisha kwamba hata watu weusi wanaweza; mmoja wao ni Uriah Rennie aliyekuwa mwamuzi wa kwanza mweusi wa soka katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Hizi hapa taarifa zaidi kutoka London, Uingereza kama zilivyoifikia TriGen Media…
Uriah Rennie, mzaliwa wa Jamaica aliyefariki dunia Juni 8, 2025 akiwa na umri wa miaka 65, anatajwa kama mtu aliyeleta mapinduzi katika dunia ya soka iliyojaa ubaguzi wa rangi kwa upande wa uamuzi, pale alipokuwa refarii wa kwanza mweusi mwaka 1997.
Kwa takriban miaka 11, Rennie alichezesha zaidi ya mechi 300, zikiwemo mechi 175 za Ligi Kuu ya England ambayo ni maarufu kwa mashabiki wa soka duniani.

Refarii wa kwanza mweusi, Uriah Rennie, mzaliwa wa Jamaica
Salamu kutoka shirika la kupinga ubaguzi wa rangi, ‘Kick It Out’ zinamtaja kama kinara katika kila namna.
“Atabaki akitambulika kama gwiji wa uamuzi ndani ya Ligi Kuu, akiwa refarii wa kwanza mweusi. Alionyesha kipaji kikubwa na kuwa hamasa kwa wengi. Uriah amechangia kwa kiwango kikubwa mwonekano wa soka unavyofahamika leo. Anapswa kushukuriwa siku zote,” wanasema Kick It Out.
EPL wanamtaja kama mwamuzi shupavu aliyefungua njia kwa wengine akiacha urithi kwa vizazi na vizazi.
Kabla ya kukumbwa na mauti, afya ya Rennie aliyekulia Sheffield, ilizorota baada ya kupooza kuanzia kiunoni kushuka chini, hivyo kulazimika kuanza upya kujifunza kutembea.
Alianza kuchezesha soka mashindano ya mitaani mwaka 1979 kabla ya kuandika historia alipochezesha mechi ya Ligi Kuu kati ya Derby County na Wimbledon mwaka 1997.
Kitaaluma, Rennie, msomi aliyekuwa na shahada ya uzamili (MBA) na sheria, alikuwa hakimu mjini Sheffield tangu mwaka 1996, akijia alijihusisha katika kampeni za usawa na ujumuishwaji michezoni, afya ya akili mapambano dhidi ya umaskini.
Novemba 2023, Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam kilimtunukia shahada ya heshima kwa mchango wake katika michezo na jamii ya South Yorkshire; baadaye akiwa Mkuu wa Chuo hicho.

Uriah Rennie akizongwa na wachezaji wa Manchester United
Chama cha Soka cha Kaunti (mkoa) ya Sheffield & Hallamshire kinamtaka Rennie, aliyekuwa mwenyekiti wake, kama mtu aliyebomoa vizingiti, akaunda jamii mpya ya soka na kuhamasisha vizazi vijavyo.
Katika mechi yake ya kwanza kama mwamuzi wa EPL, Rennie alilazimika kusitisha mchezo baada ya taa za Uwanja wa Pride Park ‘kuzimwa’.
Mwaka 2000 alipewa beji kuwa mwamuzi wa FIFA na mwaka uliofuata akajiunga na PGMOL; chama cha waamuzi wa EPL.
Akizungumza na BBC Sport mwaka 2023, mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na England, Ian Wright anasema:
“Nilipokuwa uwanjani yeye akichezesha hakuwa akizungumza na mtu! Waamuzi wengine mnaweza kuzungumza hili au lile uwanjani. Naamini hakutaka kuonekana akizungumza na wachezaji weusi (wenzake) akihofia watuu wangesema nini.”
Nje ya uwanja, Rennie anatajwa kuwa mtu mwenye heshima na mvuto kwa wengine, akiwa na mkanda mweuzi katika sanaa ya mapambano (black belt inn karate).
Mwamuzi wa zamani wa EPL, Keith Hackett, anasema: “Mara nyingi wakati wa kufanya uamuzi wachezaji wakimzunguka, alikuwa anawaambia ‘nipo hapa, nimeona’; wanabaki wakimtazama na kucheka.”

Uriah Rennie akiwa kazini
Ilichukua miaka 15 baada ya Rennie kustaafu mwaka 2008 kwa refarii mwingine mweusi, Sam Allison, kuchezesha mechi ya Ligi Kuu.
Allison alichezesha mechi ya Sheffield United dhidi ya Luton Town, Desemba 2023, mwaka ambao Shirikisho la Soka la England (FA) lilitangaza mkakati wa kuongeza uwiano wa waamuzi nchi nzima; yaani kuwa na marefarii wanawake 1,000 na weusi au wa Asia 1,000 katika ngazi zote.
Wakati mpango huo ukitangazwa, ni asilimia tatu tu ya waamuzi wa soka la kulipwa ndio waliokuwa na asili ya Kiafrika au Kiasia.