Home Kisiasa KADA CCM ATAKA UBUNGE RUNGWE

KADA CCM ATAKA UBUNGE RUNGWE

0
23

Mambo yameanza kuiva kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na sasa Jimbo la Rungwe mkoani Mbeya, limepata mtia nia ‘mpya’.

Hii hapa taarifa iliyoandaliwa na Mwandishi wa TriGen Media, Mkoa wa Mbeya, Ruja Masewa…

Ni mmoja kati ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayefahamika kwa namna anavyoishi vyema na jamii, ambaye sasa anataka kuwa mwakilishi wa wananchi bungeni.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwaiteleke Foundation, Aliko Anyambilile Mwaiteleke, mmoja wa wachangiaji wakubwa wa maendeleo, anataka kuwa Mbunge wa Rungwe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza mwishoni mwa wiki mbele ya waandishi wa habari, wanafamilia, ndugu zake na wananchi kwa ujumla, Aliko anasema atachukua fomu kugombea ubunge milango itakapofunguliwa.

“Ndugu zangu, baada ya kushirikiana nanyi katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo jimboni hapa, na ushawishi kutoka miongoni mwa wanaCCM, ninaamini kuwa ni wakati muafaka kuingia kwenye kinyang’anyilo cha kuwania ubunge wa Rungwe,” anasema.

Pazia la uchukuaji fomu ndani ya CCM linatarajiwa kufunguliwa kuanzia Juni 29, 2025 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuvunja Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

Tayari Dk. Samia amekwishapitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM huku Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiteuliwa kuwa mgombea mwenza.

Kwa upande wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi atapeperusha tena bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

“Kwa hiyo, mimi mtoto wenu na kada wa CCM; nimewaita hapa leo kuwajulisha na kutangaza rasmi kuwa nitakuwa mmoja wa wanachama wa CCM watakaoomba ridhaa ya utumishi wa jimbo hili (Rungwe),” anasema. Kwa sasa Mbunge wa Rungwe ni Antony Mwantona.

Aliko Anyambilile Mwaiteleke akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu nia yake ya kuwania ubunge Jimbo la Rungwe

Mbali na michango yake katika ujenzi wa madaraja, Aliko, alijitolea kutunza watoto wa shabiki mmoja wa Simba aliyefariki dunia kwa ajali gari na anasema udogo wa umri si sababu ya yeye kushindwa kusimamia masuala muhimu kwa wananchi.

“Nimezaliwa hapa na ninazifahamu changamoto zinazowakabili wananchi. Nia ninayo, uwezo ninao. Tusubiri muda ufike,” amesema huku akishangiliwa.

Aliko, sawa na watia nia wengine nchini, hakuwa tayari kusema lolote kuhusu mipango au vipaumbele vyake akiahidi kufanya hivyo muda utakapofika. CCM inatarajia kuanza kutoa fomu za wagombea wa ubunge na udiwani kuanzia Juni 28 hadi Julai 2, 2025 nchi nzima.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here