Juni 2, 2025 ni siku nyingine ya kukumbukwa miongoni mwa wadau wa utalii na uhifadhi nchini kwani ndiyo, kwa mara nyingine, tuzo ya kimataifa iliyotolewa na Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ilitua jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Undani wa habari hii unaletwa kwako na Mwandishi wa Masuala ya Utalii na Uhifadhi wa TriGen Media, Joseph Mwanicheta…
TANAPA, chini ya Bodi ya Wadhamini inayoongozwa na Jenerali (mstaafu) George Waitara, inaendelea kuing’arisha Tanzania kimataifa, safari hii ikitunukiwa tuzo ya ‘European Quality Choice Diamond’ 2025 katika sherehe zilizofanyika jijini Stockholm, Sweden.
Tuzo hizo hutolewa kila mwaka na taasisi ya kimataifa ya utafiti wa ubora; ‘European Society for Quality Research (ESQR)’, hii ni tuzo ya sita mfululizi kwa TANAPA.
Msafara uliokwenda Sweden kupokea tuzo uliongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, CPA Musa Kuji aliyeambatana na Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Godwell Meing’ataki na Mkuu wa Usimamizi wa Mfumo wa Ubora, Ofisa Uhifadhi Mwandamizi, Eunice Msangi.

Balozi wa Tanzanua nchini Sweden, Mobhale Matinyi (katikati) akiwa na maofisa waandamizi wa TANAPA huko Stockholm, Sweden
Walipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, huku CPA Kuji akiiinua juu tuzo hiyo, viongozi hao walipokewa na maofisa waandamizi wa TANAPA, wananchi na waandishi wa habari.
TANAPA ni shirika la umma lenye dhamana ya kusimamia, kuhifadhi mazingira na wanyamapori na kuendeleza utalii nchini.
Akizungumza mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, CPA Kuji anasema:
“Kwanza ni lazima kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutuweka hai hadi kufikia mafanikio haya; pili tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa karibu na wahifadhi wakati wote.”
Kamishna wa Uhifadhi, Kuji, mbali na kuishukuru Bodi ya Wadhamini kwa usimamizi na miongozo wanayoitoa, ameishukuru Menejimenti ya TANAPA na wafanyakazi wote.

Baadhi ya maofisa wa TANAPA wakisubiri kumpokea Kamishna wa Uhifadhi, Musa Kuji pamoja na tuzo ya kimataifa ya ubora kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam
“Huwezi kushinda tuzo hii bila kuwataja askari wetu walioko ‘site’. Hawa ndio hasa waliosababisha kupata tuzo hii,” amesema na kuweka bayana kwamba TANAPA inaitoa tuzo kwa Rais Samia kutokana na mchango wake mkubwa kwa uhifadhi.
Takriban mataifa 48 yalishindanishwa na Tanzania kuibuka kidedea kwa ngazi ya ‘Diamond’ (Almasi) katika kipengele cha uhifadhi.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Steria Ndaga, anasema TANAPA imesajiliwa ESQR ili kipima ubora wa huduma wanazotoa na hulipa ada kila mwaka.
“ESQR huwa wanatukagua na sisi kila mara tunazidisha ubora ndio maana tunashinda. Tunaahidi kuendeleza ubora wa huduma ili tuendelee kushinda,” anasema.
Naibu Kamishna Steria amewapongeza majirani wa hifadhi zilizo chini ya TANAPA na watoa huduma wengine akiamini kuwa nao wana mchango mkubwa kwa uhifadhi na kuwakirimu wageni; vitendo vilivyowawezesha kupata ushindi.
Kwa upande mwingine, Meing’ataki anasema nchini Sweden, mataifa saba ya Afrika yalishiriki na Tanzania kuibuka kidedea katika eneo la uhifadhi na utalii.

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Kuji (katikati) akiwaongoza maofisa waandamizi wa shirika hilo kutoka nje ya uwanja wa ndege. Kulia kwake ni Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Steria Ndaga na kushoto kwake ni Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Godwell Meing’ataki
“Uwekezaji wa serikali katika uhifadhi unalipa; bado tuna safari ndefu lakini ni yenye mafanikio,” anasema huku akisifu ushirikiano kati ya TANAPA na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), akisema wamesaidia kufikisha utoaji huduma wa TANAPA ngazi ya kimataifa.
TANAPA, taasisi yenye ithabiti ya ubora wa kimataifa (ISO), inaongozwa na nguzo saba ambazo ni weledi, uwajibikaji, uadilifu, ushirikiano, ufanisi, ubunifu na ubora; kwa kifupi ‘PAITEIQ’.