Tuesday, June 17, 2025
spot_img

SERIKALI KUINGIZA TRILIONI 12 UWEKEZAJI SONGWE WA BILIONI 771

Hatimaye Wizara ya Madini imeanza kutekeleza kwa vitendo wito wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuongeza thamani ya madini adimu kabla ya kusafirishwa; na Kijiji cha Ngwala kilichopo Songwe kinakuwa cha kwanza kunafaika na mkakati huo.

Hii hapa taarifa kamili kutoka TriGen Media

Usafirishaji na uuzaji wa madini adimu yakiwa ghafi unatarajiwa kukoma pale ambapo ujenzi wa kiwanda cha kusafisha na kuongeza thamani ya madini hayo mkoani Songwe kitakapokamilika.

Akizungumza wakati akizindua ulipwaji fidia kwa wananchi 192 wanaoguswa na mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (MB), amesema:

“Mradi huu, mbali na ajira, mrabaha na ushuru wa Halmashauri, utaipatia serikali mapato ya moja kwa moja ya zaidi ya Sh trilioni 12 kwa wakati wote wa uhai wa mgodi.”

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akiwapungia mkono wananchi alipowasili kwenye hafla ya uzinduzi wa ulipwaji fidia kwa wananchi wa Kijiji cha Ngwala walioguswa na mradi wa ujenzi wa kiwanda

Mamba Minerals Corporation Limited (MMCL), ndiyo kampuni inayotekeleza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha na kuongeza thamani ya madini adimu (rare earth elements – REEs) kijijini Ngwala, na ndio inayohusika katika ulipaji fidia.

‘REEs’ hutumika kwa ajili ya kutengeneza vifaa mbalimbali vya kielektroniki, hivyo kuwa miongoni mwa madini yanayohitajika sana duniani hivi sasa.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa MMCL, Ismail Diwani, amesema kiasi cha Sh bilioni 5.3 kinatarajiwa kutumika kulipa fidia kwa waguswa wa mradi.

“Kati ya waguswa 192, tayari 116 wamekwishapokea malipo yao. Hizi ni hatua za awali kuelekea katika utekelezaji wa mradi, ambapo shughuli rasmi zitaanza Desemba 2025,” amesema Diwani.

Amesema ujenzi wa mgodi utakwenda sambamba na ujenzi wa kiwanda na ujenzi wa mtambo wa kufua umeme utakaozalisha Megawati 12.

Pamoja na kuipongeza MMCL, Waziri Mavunde amewahakikishia wananchi wa Ngwala kuwa watanufaika na mradi huu mkubwa kupitia maudhui ya ndani

“Kwa namna hiyo, mradi huu utakuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wa hapa na taifa kwa ujumla,” amesema.

Mavunde amesema eneo la mradi lina wastani wa tani milioni 18.5 za mashapo (sediments) ya madini adimu hivyo kuufanya kuwa mionghoni mwa miradi mikubwa duniani ya aina hiyo ya madini.

“Kwa maana hiyo sasa Tanzania itakuwa mzalishaji wa malighafi muhimu kwa ajili ya vifaa vya matibabu, kieletroniki na ufuaji wa umeme wa upepo,” amesema Mavunde.

Mkuu wa Wilaya wa Songwe, Solomon Itunda, amesema mradi utachochea ukuaji wa sekta ya madini mkoani Songwe kwa kiwango kikubwa na kuubeba mkoa kuwa kati ya wachangiaji wakubwa wa pato la taifa kupitia sekta ya madini.

Zinazihusiana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Ungana Nasi Kupitia

0FansLike
0FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Za hivi karibuni