Ikiwa imesalia takriban miezi mitano hadi kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu 2025; Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa chama cha kwanza kitakachoshiriki uchaguzi kuzindua Ilani ya Uchaguzi.
Fuatana na Mwandishi wa TriGen Media, JOSEPH MWANICHETA, aliyeko Dodoma kwa undani wa taarifa hii…
Hayawi hayawi sasa yamekuwa. Ni kama kipyenga cha uchaguzi kimepulizwa ndani ya chama tawala, CCM, baada ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu chini ya Mwenyekiti Dk. Samia Suluhu Hassan, kuzindua Ilani ya Uchaguzi 2025.
Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unatarajiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Kifungu cha 77(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinasema: “Uchaguzi Mkuu utafanyika kila baada ya miaka mitano, au mapema zaidi kama Bunge litavunjwa kabla ya kipindi hicho kuisha.”
Kwa mara ya mwisho Uchaguzi Mkuu nchini ulifanyika mwaka 2020; hivyo tayari miaka mitano imepita, na kwa siku mbili sasa, jiji la Dodoma limekuwa na shamrashamra za aina yake kutokana na kupokea ugeni wa takriban wajumbe 2,000 kutoka kila kona ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ilani, Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dk. Samia, amesema anaamini kila kilichomo ndani ya Ilani kimepokewa vyema na wajumbe.
“Nimeisoma mara mbili Ilani hii, na nimesikiliza kwa makini ilipokuwa ikiwasilishwa hapa, ninaaminii kila mmoja ameipokea vyema,” amesema.
Awali, Dk. Samia aliwaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba kulikuwapo na wigo mpana katika maandalizi ya Ilani ya mwaka.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alimkabidhi kijitabu cha Ilani Dk. Samia ambaye ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM; pia alimkabidhi Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye ni Mgombea Kwenda na kijitabu kingine akamkabidhi Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye ni mgonbea urais wa Zanzibar.
Akifunga Mkutano Mkuu, Dk Samia amesema: “Sasa Ilani hii ni yetu sote. Ni ya Watanzania. Kila mmoja ashiriki kuwashawishi wananchi kuitekeleza. Kusiwepo migongano ndani ya chama.”
Akizungumzia mwelekeo wa uchaguzi ndani ya chama, Dk. Samia ameagiza kuwepo kwa uadilifu katika kuteua wagombea wa ubunge (na udiwani).
“Mteue watu watakaotusaidia. Msituletee watakao Gwajamanise chama chetu,” amesema, akirejea kauli zilizotolewa na kada wa CCM, Askofu Josephat Gwajima wiki iliyopita, zilizoikosoa serikali ya CCM kuhusu masuala mbalimbali.