James Ngugi huenda linaweza kuwa jina geni kidogo kwa wafuatiliaji wa kazi za Kifasihi lakini Ukisema Ngũgĩ wa Thiong’o, kila mfuatiliaji wa vitabu vyake atajua kwamba ni yule Nguli katika kazi za kifasihi ambaye katika makala hii mbali ya kukutangazia kifo chake lakini utakwenda kusikia wasifu wake na kazi zake ambazo zilimtambulisha Afrika na duniani kwa Ujumla.
Ngugi wa Thiong amefariki Dunia ni taarifa zilizoanza kusambaa katika mitandao ya kijamii Mei 29.2025 na ndipo taarifa kuanzia Kenya zikasambaa maeneo mengine Afrika na sasa Duniani.
Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87. Alizaliwa mwaka 1938 wakati huo Kenya ikiwa chini ya utawala wa Kikoloni wa Muingereza.
Alikulia na kulelewa katika familia ya kawaida kabisa,ya wakulima wadogo ila katika familia kubwa kwa idadi ya wanafamilia.
Kama ilivyo kwa familia za hali ya kipato cha chini Ngugi wa Thiong’o pia wazazi wake walilazimika kijibana na kuhakikisha wanamudu gharama za kumlipia masomo yake katika ngazi tya sekondari kwenye shule ya Alliance, iliyokuwa shule ya bweni chini ya wamishonari wa Kiingereza.
Mwaka 1959, Ngũgĩ aliondoka nchini Kenya na kwenda masomoni nchini Uganda ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere,chuo kikuu cha hadhi ya juu wakati huo hadi sasa.
Ngũgĩ aliandika riwaya yake ya kwanza kwa ushirikiano na mwandishi Nguli wa Nigeria Chinua Achebe.
Achebe alipeleka riwaya nchini Uingereza kwa mchapishaji wake na kitabu hicho, kikatoka kwa jina la Weep Not, Child, chapisho lake la kwanza ikawa mwaka 1964. Ilikuwa ni riwaya ya kwanza kuu ya lugha ya Kiingereza kuandikwa na raia wa Afrika Mashariki.
Hata hivyo Riwaya hiyo ilikata utepe kwa ujio wa riwaya nyingine mbili ndani ya muda mfupi ambazo ni A Grain of Wheat na The River Between,na mwaka 1972, akatambuliwa rasmi na gazeti la Times la Uingereza kuwa mmoja wa mwandishi bora akiwa kijana mdogo wa miaka 33 wa Afrika.

Alikuwa ni mzalendo kweli kweli na Afrika hata jina lake la Ngugi ilikuwa kama kugonga muhuri uzalendo wake na kuachana na jina la kizungu yaani James ikiwa ni vuguvugu la kimapinduzi ndani yake.
Yapo baadhi ya matukio yaliyochochea harakati za kimapinduzi kupitia Fasihi kwa Ngugi kama vile aliposhuhudia kaka yake Gitogo akipigwa na risasi baada ya kutotii amri ya askari wa Kiingereza. Hata hivyo iliumiza mioyo ya wengi akiwemo Ngugi mwenyewe kwa sababu kaka yake hakuisikia amri hiyo kwa kuwa alikuwa kiziwi.
Na ukipitia kazi zake za Kifasihi utagundua kwamba vilikuwa ni vya kimapinduzi zaidi kwani baadhi vilikuwa vinakosoa serikali ya kikoloni, huku maudhui ya Riwaya ya Petals of Blood ikishambulia viongozi wapya wa taifa la Kenya baada ya uhuru, na kuwaonyesha kama tabaka la wasomi ambao walikuwa wamesaliti Wakenya wenzao wa kawaida.
Ngugi huyu kazi zake ziliwahi mtia matatani na shughuli zake za kutaka kuigiza zilizuiwa na serikali ya Kenya wakati huo na akafungwa jela chini ya utawala wa Jomo Kenyatta.
Zipo panda shuka nyingi alizopitia Ngugi wa Thiong’o ambaye baadhi ya vitabu vyake vimetumika na vinatumika katika mitaala ya kufundishia si Kenya tu bali na kwingineko Afrika kama vile kitabu cha River Between,Devil on the cross,Matigari,A grain of wheat,Petals of Blood na vinginevyo havitasahaulika daima kuwekwa katika kazi bora kabisa za kifasihi.Nenda Salama Ngugi wa Thiong’o