Tuesday, June 17, 2025
spot_img

Dk Tax: Vijana msiwe na haraka

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax ametoa mwito kwa vijana wasiwe na haraka ya kupanda katika nafasi za uongozi.

Dk Tax alisema hayo alipozungumza katika kituo cha televisheni cha TBC Digital cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) juzi.

Alisema alianza kazi akiwa ofisa wa ngazi ya chini na aliwajibika kwa weledi katika majukumu yake na akawa mvumilivu.

Nilianza kazi ofisa wa chini kabisa serikalini nikajituma nikapanda hatua kwa hatua, usisahau una wakubwa wako wa kazi, wanakukosoa uwe tayari kupokea na ujifunze na uwe tayari kupewa majukumu mengine bila kuchoka na usiseme si kazi yangu,” alisema DkTax.

Aliongeza: “…Vijana wanapenda kwenda haraka sana, vumilieni, uvumilivu ni kitu muhimu sana, ukivumilia kazi inakujenga na kukupa nafasi zaidi. Jiulize niko kwenye hili shirika madhumuni yangu ni nini mchango wangu ni upi ndani ya shirika?”

Dk Tax ameishukuru serikali kwa kuwa amekuwa mtumishi wa umma tangu alipomaliza shule na baada ya kuingia serikalini aliendelea kujengwa na kupata fursa za kuendelezwa kielimu na serikali ambayo pia, ilimjengea uwezo na kushika nafasi ndani na nje ya nchi.

Alisema katika safari yake ya utumishi serikalini, anajivunia kuwa mmoja wa waanzilishi wa mfumo wa stakabadhi ghalani unaoendelea kutumika na kusaidia wakulima hadi sasa.

Pia, anajivunia kuwa miongoni mwa watunga sera zinazotumika nchini, hata katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Dk Tax alisema alipoteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa SADC, alikuta jumuiya hiyo haijasajiliwa katika Umoja wa Mataifa (UN) ndipo alitekeleza wajibu wake na baada ya miaka miwili ilisajiliwa rasmi.

“Niwaambie wanawake wengine, ukiaminiwa na kupata nafasi ya kuhudumu, fanya kazi kwa weledi, kwa sababu changamoto zipo na zinampata kiongozi wa kike au wa kiume, lakini msingi ni kufanya kazi ili uwezo wako uonekane,” alisema.

Aliongeza: “Ila changamoto nyingi tunazishinda, waoneshe unaweza na fanya kazi zako kwa kujiamini, huwa zinaisha, ingawa watakujaribu tena ila jiamini wataacha”.

Dk Tax ameshauri wanawake wajiamini, wafuate misingi ya kisheria na taratibu na siku zote wanyooke kwenye haki na kuthamini timu wanayofanya nayo kazi.

Alisema ujasiri na udhubutu ameupata kutoka kwa mama yake ambaye kitaaluma ni mwalimu. Alisema kuwa watoto wa walimu wengi wao wana uthubutu.

“Ilikuwa kuna wakati mama anakuadhibu unabaki unasema hivi huyu ni mama yangu kweli, tulifanya kazi kwa usawa bila kujali jinsi, mama alitusimamia ndiyo maana tumefika hapa tulipo leo,” alisema Dk Tax.

Amesema anajivunia kuwa katika nafasi alipo sasa kwa kuwa nchi ilipata uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita lakini wizara hiyo haikuwahi kuongozwa na waziri mwanamke.

“Namshukuru Mungu na wazazi wangu walioona umuhimu wa kuniendeleza kielimu… namshukuru sana, Rais Samia Suluhu Hassan ndiye aliyevunja kizingiti na mimi kushika wadhifa huu. Hii inatoa picha halisi kuwa wanawake wanaweza kufanya kazi sehemu yoyote bila kujali jinsi,” alisema Dk Tax.

Zinazihusiana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Ungana Nasi Kupitia

0FansLike
0FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Za hivi karibuni